Sunday, January 1, 2012

Wannje huona mzuri

Yanishangaza tabia ujinga ilivyokuwa,
Ndani unawanunia, wannje unawachekea,
Wale wanaokufaa, wakawa kwako udhia,
Wannje huona mzuri, ndani hauna maana.

Ndani ulimi waua, mdomo hujiozea,
Huna unalosikia, kila kitu unajua,
Wenzi wanapoumia, pengine wafurahia,
Wannje huona mzuri, ndani hauna maana.

Furaha huiondoa, nyumbani unapokaa,
Kwingine kuichukua, tena usikokujua,
Waacha wana walia, wa wengine wawalea,
Wannje huona mzuri, ndani hauna maana.

Marafiki wachukua, siku waliozidia,
Ujinga wakufundia, nawe unauchukua,
Mwenyewe wajiibia, wala usiwe na haya?
Wannje huona mzuri, ndani hauna maana.

Mzuri wa kutumiya, kwa yasiyokusaidia,
Hata ndani kufagia, kazi kubwa inakuwa,
Mapambo hujayajua, somo hakukuambia,
Wannje huona mzuri, ndani hauna maana.

Huwezi ukatulia, jema ukaliongea,
Kazi nje kukimbilia, kushika yasiyokufaa,
Marafiki wakutumia, wewe hujawajua,
Wannje huona mzuri, ndani hauna maana.

Nduvu wajiovunia, kupe waliokuvaa,
Na ukubwa wadhania, kuna siku utapewa,
Waishi kwa kuotea, goli hutojipatia,
Wannje huona mzuri, ndani hauna maana.

Huambiwa warejea, taadibu kusikia,
Hatua wakachukua, wenyewe wakajijua,
Wafanze yanayofaa, kwao na zao familia,
Wannje huona mzuri, ndani hauna maana.

Mustakabali ukiwa, ndivyo utakavyokua,
Huwezi kuukimbia, nabii walijikwaa,
Ila ninachokijua, haya yatakuumbua,
Wannje huona mzuri, ndani hauna maana.

Ushauri inafaa, ukubali kuchukua,
Iache hiyo tabia, nyumba kuiangalia,
Vya ndani kuvinyanyua, vije kukusaidia,
Wannje huona mzuri, ndani hauna maana.

Hakika ninakwambia, furaha hutoijua,
Nje kuikimbilia, hiyo njozi na ruia,
Furaha ya kweli huwa ndani yako inayokaa,
Wannje huona mzuri, ndani hauna maana.

No comments: