Tayari nilishasema, mkafunga masikio,
Watu walia ujima, na sio msikiao,
Hawanayo takrima, njaa tupu nyimbo yao,
Sifa ya kilichooza, kwa dakika huja nuka~!
Afueni walalama, ndio kubwa kiu yao,
Wenyewe mnajinoma, hamujui hali zao,
Kwao kwazuka kiyama, hawajui kesho yao,
Sifa ya kilichooza, kwa dakika huja nuka~!
Viumbe wafa wazima, walia na nchi yao,
Wanaukosa uzima, hali ardhi ni yao,
Na sasa pia heshima, nayo sio shani yao,
Sifa ya kilichooza, kwa dakika huja nuka~!
Tazama mnachosema, ngumu dunia ya leo,
Zitawavunja kalima, mme wawachukiao,
Kwa hasira kuwazoma, muwe matapishi yao,
Sifa ya kilichooza, kwa dakika huja nuka~!
Msikione kizima, mkawa ni waringao,
Yataka sana hekima, hamuyaoni ya moyo,
Mabomu yanarindima, yangoja wateguao,
Sifa ya kilichooza, kwa dakika huja nuka~!
Naichelea nakama, za mbuni wajifichao,
Wasiotaka rehema, toka kwa wanyonge wao,
Wajifanyao Obama, na ardhi sio yao,
Sifa ya kilichooza, kwa dakika huja nuka~!
Sunday, January 1, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment