MKOPO ujana jua, unakuja kudaiwa,
Ukishindwa kutumia, mazuri kujichumia,
Mwishoni utahojiwa, nini kilichotokea,
Ujana jua mkopo, utakuja daiwa!
Inafaa kufungua, akili ulizopewa,
Asubuhi kutambua, deni lako linakua,
Lisije kukulemea, ukashindwa kulipia,
Ujana jua mkopo, utakuja daiwa!
Wazazi wasiojua, wewe wakakuachia,
Vyema kuwahurumia, kwingine ukayavua,
Muhimu yaliyokuwa, kesho yako kuandaa,
Ujana jua mkopo, utakuja daiwa!
Manani kakuandaa, wengine kutumikia,
Si mwenyewe kujifaa, huo uhayawani huwa,
Molawe kumrudia, jukumu hili chukua,
Ujana jua mkopo, utakuja daiwa!
Kisha dini kuijua, haya inayoyajua,
Ukasoma na kujua, kitu gani watakiwa,
Na kisha ukajitoa, kufanya sabili laha,
Ujana jua mkopo, utakuja daiwa!
Saturday, January 7, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment