Saturday, January 7, 2012

Maisha ni kutafuta, na sio kutafutana !

Haya watu wateta, kuvumbua langu sina,
Ni bure ukinisuta, hekima mpaka haina,
Na mie ninaileta, ukweli wake kuona,
Maisha ni kutafuta, na sio kutafutana !

Maisha ni kupepeta. wala si kusagishana,
Yataka kamba kuvuta, na sio kuburuzana,
Na mtu asiyeleta, haupati uungwana,
Maisha ni kutafuta, na sio kutafutana !

Maisha si kupakata, ila ni kupatikana,
Heri kinachoileta, nyumba ije tulizana,
Umoja unaonata, mkawa mnaungana,
Maisha ni kutafuta, na sio kutafutana !

Maisha sio kuteta, na watu kubibizana,
Mkawa kuzusha vita, mwache kuendelezana,
Dunia huja wasuta, wa ovyo kuonekana,
Maisha ni kutafuta, na sio kutafutana !

Maisha sio karata, na nasibu kuikuna,
Bahati ni kutafuta, sio kubahatishana,
Haujengeki ukuta, bila tofali kubana,
Maisha ni kutafuta, na sio kutafutana !

Iwe kheri kutafuta, Yahilahi yarabana,
Tuondolee matuta, mwakani tuvune sana,
Mchele nao ufuta, bei ziache pishana,
Maisha ni kutafuta, na sio kutafutana !

No comments: