Saturday, January 7, 2012

Udugu si kufanana

Angelipenda msana, sote tungelifanana,
Tukawa kama Machina, pasi kutofautiana,
Ila bora kaiona, wajihi kutolingana,
Udugu si kufanana, udugu ni kufaana!

Wa chini na juu sana, hata hivyo hufaana,
Ndivyo inavyotakikana, kasema ya Rabana,
Na walo waungwana, hili wanahimizana,
Udugu si kufanana, udugu ni kufaana!

Ndugu wasiofaana, si ndugu ila laana,
Dhiki kushirikiana, hata na kuuguzana,
Sembuse kukopeshana, wapate saidiana?
Udugu si kufanana, udugu ni kufaana!

Wa nje bora huona, si ndugu wa muamana,
Mabaya watayanena, ndugu wote kuwakana,
Huku buzi wanachunwa, na wanaoaminiana,
Udugu si kufanana, udugu ni kufaana!

Waafrika ndio sana, hili kwetu ni laana,
Ubaya twazidiana, ndugu tunavyotendeana,
Wageni huja kupona, kwa sisi tunavyouzana,
Udugu si kufanana, udugu ni kufaana!

Watanzania hunena, ndugu hawana maana,
Wengi hutelekezana, wakaacha kujuana,
Hawana wanachovuna, ila wanapozikana,
Udugu si kufanana, udugu ni kufaana!

Yafaa kuhimizana, tabia hii kuguna,
Haifai kwetu tena, tuacheni kuuzana,
Tuweze saidiana, kheri tuje kuiona,
Udugu si kufanana, udugu ni kufaana!

Tuache kununiana, tuanze kusemezana,
Nchi haiwezi nona, ikiwa hatutanona,
Watu tusipojengana, taifa nani kusana?
Udugu si kufanana, udugu ni kufaana!

No comments: