Saturday, January 7, 2012

Amani ni kugawana, sio kulazimishana!

HERI kusaidiana, na watu wakabebana,
Huruma kuoneana, katutaka Maulana,
Na kisha kuaminiana, na kuendelezana,
Amani ni kugawana, sio kulazimishana!


Watu wanapopeana, eti kwa kufahamiana,
Na wasiojulikana, wabaki watafutana,
Amani nje huona, na bora pafaa sana,
Amani ni kugawana, sio kulazimishana!

Wachache wakijichana, na wengi wakamiana,
Njaa inaponong'ona, na meno yakasagana,
Pasiwe kuaminiana, amani hutoiona,
Amani ni kugawana, sio kulazimishana!

Mwongo anapojiona, ukweli ajua sana,
Na mkweli akabanwa, muongo kuonekana,
Ndimi zinapong'atana, amani husagikana,
Amani ni kugawana, sio kulazimishana!

Viongozi wakinona, na wananchi kukondeana,
Tofauti kubwa sana, huja ikaonekana,
Hata wakisemeshana, hakuna kusikilizana,
Amani ni kugawana, sio kulazimishana!

Wanapopendeleana, madaraka walotuna,
Wengine kuwa laana, na wao kuepukana,
Na wasioonekana, na mfumo huvaana,
Amani ni kugawana, sio kulazimishana!

Na mahali penye kina, madini yakazaana,
Na wenyeji kutovuna, kilicho kwao maana,
Dunia wataichana, hadi haki kuiona,
Amani ni kugawana, sio kulazimishana!

Wawao wajinga sana, ujuzi huja vuna,
Dhuluma wakiiona, hasira huzaliana,
Na yanayofuatana, stori husimuliana,
Amani ni kugawana, sio kulazimishana!

No comments: