Umoja hutengenezi, wenyewe unachanua,
Pasipo na walanguzi, watu wanaolalia,
Na mzigo shehenezi, bure inayonyanyuliwa,
Umoja unachanua, wala hautengenezwi!
Nafsi zilizo hadhi, utu zinazoujua,
Huwa kwao sio kazi, umoja kutengania,
Ila katu sio wezi, vya watu wanaochukua,
Umoja unachanua, wala hautengenezwi!
Umoja una mizizi, kati ya watu tabia,
Waenzio chapakazi, na haki wakaitoa,
Sio wenye uteuzi, uoza wakachagua,
Umoja unachanua, wala hautengenezwi!
Umoja bila makazi, haujawahi tokea,
Watu huwa walowezi, pembeni wakafagiwa,
Huyafanya machukizi, wengine wakachukia,
Umoja unachanua, wala hautengenezwi!
Umoja kwenye maradhi, uhai yanayotwaa,
Ni hayati kwa malazi, marehemu keshakua,
Ipi aifanze kazi, ya kuja kukusaidia?
Umoja unachanua, wala hautengenezwi!
Umoja bila malezi, wana wakahudumiwa,
Huwa ni kubwa ajizi, yajayo kuwatokea,
Huwezi panda viazi, mpunga ukajaliwa!
Umoja unachanua, wala hautengenezwi!
Mafisadi fumanizi, umoja huuchukia,
Hoja zao za mandazi, na fikra vitumbua,
Si wa jana ni wajuzi, kwa watakayokwambia,
Umoja unachanua, wala hautengenezwi!
Na wanasiasa wezi, kazi yao ni kugawa,
Hufumua ufumuzi, vipandepande vikawa,
Ya kwao kupanda ngazi, ya chini wanakataa,
Umoja unachanua, wala hautengenezwi!
Huiba kwa kina Juma, John wakampatia,
Humjenga Mwanaima, Maria akaibiwa,
Ndivyo chama na dhuluma, hustawi na kukua,
Umoja unachanua, wala hautengenezwi!
Stihizai Karima, yote hii waijua,
Wape yao waadhama, ya kwetu kuyaokoa,
Mbizi kuishia zama, ni jambo hutarajiwa,
Umoja unachanua, wala hautengenezwi!
Saturday, January 7, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment