Uhuru ninaojua, uhuru wa kufa njaa,
Nani kuniangalia, bei zinazonipalia,
Naitesa familia, kwa vibaba visojaa,
Uhuru ninaojua, ni uhuru wa ukata!
Uhuru ninaojua, ule wa kukosa kazi,
Elimu nimeshapewa, ajira ni masimulizi,
Niipataje hifadhi, katika hii ajizi,
Uhuru ninaojua, ni uhuru wa ukata!
Uhuru ninaojua, uhuru kukosa maji,
Sasa vita imekua, maji sawa na theluji,
Vipi nitauvamia, Kilimanjaro kuhiji,
Uhuru ninaojua, ni uhuru wa ukata!
Uhuru ninaojua, mikopo ninayonyimwa,
Vizito waichukua, miye huku nasakamwa,
Hili ningelitambua, kuzaliwa ningekoma,
Uhuru ninaojua, ni uhuru wa ukata!
Uhuru ninaojua, kutapanywa biashara,
Machinga nadhulumiwa, sina ila mbaya bishara,
Uhuru niliopewa, uhuru wenye hasara,
Uhuru ninaojua, ni uhuru wa ukata!
Uhuru ninaojua, nyumba kwangu ni anasa,
Hekalu wazinyanyua, miye maisha mkasa,
Huruma wa kunionea, ni mamba wa kisiasa,
Uhuru ninaojua, ni uhuru wa ukata!
Uhuru ninaojua, kufa na site kuzikwa,
Ugonwa ukinivaa, spitali sintawekwa,
Shilingi sijaijua, kwa dawa nitaepukwa,
Uhuru ninaojua, ni uhuru wa ukata!
Uhuru ninaojua, wa kukaa kwenye giza,
Popo wakanipepea, na kuona mauzauza,
Nisijue yakujua, ujinga nikauoa,
Uhuru ninaojua, ni uhuru wa ukata!
Uhuru ninaojua, FFU kuvamia,
Maandamano ikiwa, na machozi kunitoa,
Haki kujielezea, si uhuru ulokua,
Uhuru ninaojua, ni uhuru wa ukata!
Uhuru ninaojua, kuzungumza kuzuiwa,
Kukutana kujikwaa, na umoja kuung'oa,
Mishipa yazidi pwaya, na boila zinajaa,
Uhuru ninaojua, ni uhuru wa ukata!
© 2011 Sammy Makilla
Sunday, January 1, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment