Sunday, January 1, 2012

Paka wa Sultani

Paka wa mheshimiwa, naye ni mheshimiwa,
Awe shume tena duni, angali mheshimiwa,
Atatamba mitaani, kwa wenzaake hayawani,
Paka wake Sultani, na yeye Sultani!

Utu kitu cha hisani, mwerevu atabaini,
Utukufu hathamini, ajiongeze thamani,
Hujishusha sana chini, akawa ni mtu duni,
Paka wake Sultani, na yeye Sultani!

Ila kama afkani, hujikweza ardhini,
Juu anaposakini, mwishowe hufichwa ndani,
Tambo na zake razini, ziwe hazina auni,
Paka wake Sultani, na yeye Sultani!

Nafsi kuwazaini, pepo iko duniani,
Nyota wakaziamini, na kuwapa tumaini,
Ila siku ikighani, hujikuta majinuni,
Paka wake Sultani, na yeye Sultani!

Ni mapaka machakani, yasiyo nayo imani,
Wenyewe hujizaini, kwa yaliyo akilini,
Wasojua kwa yakini, vyote huishia chini,
Paka wake Sultani, na yeye Sultani!

Paka wake sultani, hujiongezea shani,
Utukufu kubaini, na ubora kuamini,
Akajiona peponi, wakati yu duniani,
Paka wake Sultani, na yeye Sultani!

Haya sikusimuliwa, ila nimejionea,
Na kila nikichunguwa, nazidi kulielewa,
Ila wanaopitiwa, sio wanaojijua,
Paka wake Sultani, na yeye Sultani!

© 2011 Sammy Makilla

No comments: