Friday, January 6, 2012

Ubinafsi balaa.

NDIO tuliowachagua, na sasa washupalia,
Mradi umeshakua, njaa kali inaua,
Hata ndugu nao pia, mtihani huingia,
Ubinafsi balaa.

Nafsi juu zapaa, ushindani waingia,
Mtu hana wa kumjua, ila kuganga yake njaa,
Makubwa ananuia, hata wengine kuua,
Ubinafsi balaa.

Mashindano yamekua, panya wanayokimbia,
Na wanakoelekea, hakuna anayejua,
Baharini hutokea, yakawa ni majaliwa,
Ubinafsi balaa.

Kukufuru inakuwa, kufa wanakatalia,
Ni wajinga wanakuwa, kifo wanaochagua,
Na wao wanajitia, werevu kuuambaa,
Ubinafsi balaa.

Hupanga wakadhania, yao yote yatakuwa,
Miaka kushadidia, watakayo kutokea,
Na wanavyokujajaliwa, kiburi huwazidia,
Ubinafsi balaa.

Watoto wanavyolea, aushi utaidhania,
Milele wamezaliwa, dunia hii kukaa,
Izraili ashgaa, kiburi kilivyokuwa,
Ubinafsi balaa.

Ya kwao huamkia, wakayachangamkia,
Asubuhi hata huwa, hilo hawahofia,
Ya wengine huzubaa, hadi miaka ikawa,
Ubinafsi balaa.

Hata niliowadhania, huko huko waelekea,
Nani wa kumwambia, kusimamisha hatua,
Huenda nimepagawa, wengi watanidhania,
Ubinafsi balaa.

Ila mikosi najua, mingi inajiandaa,
Yapenda kutembelea, hivi wanaoishia,
Huja ikawazingua, wasiamini nazaa,
Ubinafsi balaa.

No comments: