Friday, January 6, 2012

Hupewa wenye nasaba.

Msaada hugaiwa, kwa walioteuliwa,
Nasaba wakiijua, na chama kushahadia,
Ndipo jina watatia, sehemu ukachukua,
Misaada Tanzania, inafaa kutambua:
Hula walokwishashiba.

Wewe wasiyekujua, hesabu hujapangiwa,
Miaka utangojea, afu hautoijua,
Jua hukuangazia, hadi likakushukia,
Siku unayotegemea, tarehe haikutiwa:
Hupata walionona.

Historia yatwambia, walonacho hujaliwa,
Wasonacho haijawa, siku moja kutokea,
Ni hadithi twasikia, kweli hatujaijua,
Na kama watongopea, Mola tunamwaachia:
Hupata walichonacho.

Ya kwao ukitikia, ndipo wanapokujua,
Utumwa ukiingia, wa maana utakuwa,
Makombo utamwagiwa, nafisi kufurahia,
NI kinyemi chawa kipya, hauishi kupagawa:
Huvipata lambalamba.

Kama mke haukuwa, au mume muolewa,
Au mwana kuzaliwa, nasaba kujipatia,
Sahau nakwambia, jina halitoingia,
Kapu nenda kuchukua, kuvuna nimeamua:
Hupewa wenye nasaba.

No comments: