Ukijifanya wajua, tena unajua huu,
Wenzio huwa wajua, uliojuu wa unhuu,
Wazo lako hupindua, kichwa chini ja kifuu,
Ukijifanya wajua, wenzio wajua unhuu!
Halali iliyokuwa, haramu kama tambuu,
Majigambo hujitia, ya unanga na bahau,
Kaida husimulia, kama ajabu ikawa,
Ukijifanya wajua, wenzio wajua unhuu!
Madaraka mwanandaa, mwenye njaa hutambua,
Na tumbo lisougua, haliwezi jisugua,
Na nazi iliyovia, tui haiwezi toa,
Ukijifanya wajua, wenzio wajua unhuu!
Ukitezea sheria, hutangua vitunguu,
Na milima isokuwa, haiwezi kuwa nguu,
Na juu mnapokuwa, inda haziwasahau,
Ukijifanya wajua, wenzio wajua unhuu!
Babu anapolia, hawezi kuwa mjukuu,
Huwa jambo kaotea, pia kaona mafuu,
Nayo humuashiria, asoweza kudharau,
Ukijifanya wajua, wenzio wajua unhuu!
Utu ni njema tabia, hayayapendi malau,
Nyota waliojaliwa, hudhani waenda juu,
Chini hutaka kimbia, ila mbawa husahau,
Ukijifanya wajua, wenzio wajua unhuu!
Hekima walojaliwa, hutaliki ubahau,
La kufanya hulijua, lisiolokuwa malau,
Wakatenda kutanzua, kwa vifungu na nahau,
Ukijifanya wajua, wenzio wajua unhuu!
Friday, January 6, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment