Friday, January 6, 2012

Neema

Mengi waja twajaliwa, katika hii dunia,
Laiti tungelijua, shukrani tungetoa,
Na kumhimidia, si' anayetuangalia,
Neema ukikufuru, ni mikosi na maradhi.

Ila wengi twaumia, kwa kutoyafikiria,
Mazuri tunapopewa, yetu huwa twadhania,
Na aliyetugaiya, huwa tunamkataa,
Neema ukikufuru, huleta maangamizi.

Neema yenye ulua, shukrani hutambua,
Na kila linaloingia, sadakaye hutolewa,
Na waliopungukiwa, hawaachi saidiwa,
Neema ukishukuru, ni amani na mapenzi.

Muumba hufurahia, na yeye akisifiwa,
Heshima kumiminiwa, wajue wasomjua,
Baraka hupalilia, kila mahala kujaa,
Neema ukishukuru, ni mola hukuongezea.

Hili nimeling'amua, nami nalishikilia,
Siwezi kuliachia, kimya nafuatia,
Siku iliyoahdiwa, nami nitaingojea,
Neema ukikufuru, ni mikosi na maradhi.

Mola nitamlilia, hadi akanisikia,
Dua kuzimiminia, hadi pomoni kujaa,
Malaika kuchukua, na akiba wakatwaa,
Neema ukikufuru, huleta maangamizi.

Kizazi kunijalia, nyuma kikafuatia,
Uweledi kilojaa, na Mola awatangulia,
Na njia wanazo0pitia, ziwe zinabarikiwa,
Neema ukishukuru, ni ni amani na mapenzi.

Hofu ninaiondoa, ulinzi uliokua,
Wasiwasi nautoa, upendalo hutimia,
Nami ukinijalia, sadaka nitajaliwa,
Neema ukishukuru, ni mola hukuongezea.

No comments: