Thursday, January 5, 2012

Hudanganyika

Wapendwa ukiamini, basi huzainika,
Hudhani una thamani, kumbe kumbe mbuzi watumiwa,
Huchunwa hadi kichwani, raha ukifurahia,
Ukiamini Wapendwa, basi utadanganyika.

Hakuna yake mizani, mapenzi kuyapimia,
Ruia huwa moyoni, mtu ukayawazia,
Ukajipa na thamani, pendo likikubaliwa,
Ukiamini Wapendwa, basi utadanganyika.

Mjini kuna wahuni, kudanganya wanajua,
Huwatavuta afkrani, wakawaigilizia,
Mchezo wakiamini, ni kweli iliyokuwa,
Ukiamini Wapendwa, basi utadanganyika.

Watayavuna mapeni, huku pendo unalewa,
Yakiisha mfukoni, lazima kukutimua,
Hukuona sasa nyani, tena na mkubwa mkia,
Ukiamini Wapendwa, basi utadanganyika.

Mlio unywamwezini, nyumbani mngetulia,
Na Wachagga mamndenyi, hadaa yawangojea,
Hudakwa Kiboroloni, washindwe panda Kidia,
Ukiamini Wapendwa, basi utadanganyika.

Naliota jasmini, ua lililopotea,
Nilitulia shambani, mji nikaukimbia,
Ila haikuwa shani, mkiwa sikujaliwa,
Ukiamini Wapendwa, basi utadanganyika.

Hubisha wenye auni, maisha yanayofaa,
Na wengi wanaamini, bila pendo ni balaa,
Ila vigumu yakini, mapenzi kuyagundua,
Ukiamini Wapendwa, basi utadanganyika.

No comments: