Haramu utaitema, ndugu yangu nakwambia,
Kijapofika kiyama, maswali ukatupiwa,
Hivyo iwe ni nakama, haramu kuivamia,
Ni vipi umeichuma,na vipi umetumia:
Mali yako ni mkopo, maswali utaulizwa!
Halali kuitazama, ni mkubwa ushujaa,
Uzikubali lawama, kuchekwa na kutaniwa,
Ila usirudi nyuma,halali kuitambua,
Ni vipi umeichuma,na vipi umetumia:
Mali yako ni mkopo, maswali utaulizwa!
Iombe yake neema, vizuri kuitumia,
Yasije yakakukwama, maswali yakikujia,
Usifanye ya zahama, na sifa kujitakia,
Ni vipi umeichuma,na vipi umetumia:
Mali yako ni mkopo, maswali utaulizwa!
Swali hili la lazima, maksi linachukua,
Karibu ni nusu nzima, ya zote zilizokuwa,
Na kuzipata alama, kujituma watakiwa,
Ni vipi umeichuma,na vipi umetumia:
Mali yako ni mkopo, maswali utaulizwa!
Saturday, January 7, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment