Saturday, January 7, 2012

ELIMU yako mkopo.

ELIMU ukijaliwa, hilo ni deni tambua,
Yafaa kuitumia, kwa yale yatayokufaa,
Siku zikishatimia, thawabu kujivunia,
ELIMU yako mkopo!

Naam utashangaa, haya ukiyasikia,
Bali nakuhakikishia, ni ukweli ulotimia,
Kama hukuyajua, macho nimekufungua,
ELIMU yako mkopo !

Ni deni ninakwambia, utakuja kudaiwa,
Muumba unayemjua, budi kuliulizia,
Nawe kumsimulia, jinsi ilivyokuwa,
ELIMU yako mkopo !

Askari hudaiwa, na wao pia raia,
Ole wao watumiwa, na hawatasaidiwa,
Kila wakisingizia, kidole kwa hurejea,
ELIMU yako mkopo !

Nguvu waliotumia, wanafunzi kuwavaa,
Au wapole raia, waliojikutania,
Na maandamano yakawa, salama yenye ulua,
ELIMU yako mkopo !

Husimulia jamaa, kisha kuhukumiwa,
Elimu waliitumia, vibaya isivyofaa,
Motoni wataingia, huku wakijijutia,
ELIMU yako mkopo !

Wahadhiri wasofaa, za ndani wanaovua,
Nao watasimulia, huku ukiwa wakiwa,
Wasiamini kujua, wenye aya wayajua,
ELIMU yako mkopo !

Na walimu nao pia, kitabu kitasogea,
Muda hawakutumia, wanafunzi kuandaa
Ni yao wlaijifanyia, fedha wakifukuzia,
ELIMU yako mkopo !

Wanasiasa wakiwa, zamu itawafikiya,
Midomo itanyamaa, la kujibu kutojua,
Midomo itaamua, yenyewe kujisemea,
ELIMU yako mkopo !

Elimu waliyopewa, wenyewe walitumia,
Kingi wakajimegea, chakula kilichokuwa,
Dhuluma wakaamua, vya watu kuvichukua,
ELIMU yako mkopo !

No comments: