Tuesday, March 27, 2012

Wanaonunuliwa

Vibarakala si jana, ndipo walipoanzia,
Hawa ni yetu amana, huifuata dunia,
Kazi yao ni utwana, mabwana kutumikia:
Kila anayetumiwa, kwa hiari yake mwenyewe,
Moto anauchochea
Hawezi kusamehewa
Nadra ataombewa
Hata na anayemtumia
Jehanamu huingia!

Kwenye redio wajaa, huru na zinazotumiwa,
Kazi yao kutumiwa, uongo waupakua,
Matunda yake twajua, Rwanda tulijionea,
Kila anayetumiwa, kwa hiari yake mwenyewe,
Moto anauchochea
Hawezi kusamehewa
Nadra ataombewa
Hata na anayemtumia
Jehanamu huingia!

Magazeti nayo pia, wengi wananunuliwa,
Huajiri changudoa, ili mradi kuwafaa,
Malengo yakatimia, bei rahisi ikawa,
Kila anayetumiwa, kwa hiari yake mwenyewe,
Moto anauchochea
Hawezi kusamehewa
Nadra ataombewa
Hata na anayemtumia
Jehanamu huingia!

Huandika yasokuwa, wakaacha yalokuwa,
Vigumu kununuliwa, ila ruzuku huvua,
Samaki uozo hua, kutupwa wakiamkia,
Kila anayetumiwa, kwa hiari yake mwenyewe,
Moto anauchochea
Hawezi kusamehewa
Nadra ataombewa
Hata na anayemtumia
Jehanamu huingia!

Televisheni kwingia, haraka wazikimbilia,
Kinyaa waliokuwa, marashi kujipakaa,
Na udi kujitia,ubani kuvukizia,
Kila anayetumiwa, kwa hiari yake mwenyewe,
Moto anauchochea
Hawezi kusamehewa
Nadra ataombewa
Hata na anayemtumia
Jehanamu huingia!

Uoza ukishakuwa, vigumu ukarejaea,
Freshi haijakuwa, na wala haitakuwa,
Uoza ukishakua, hivyohivyo hubakia,
Kila anayetumiwa, kwa hiari yake mwenyewe,
Moto anauchochea
Hawezi kusamehewa
Nadra ataombewa
Hata na anayemtumia
Jehanamu huingia!

Labda ukishakaukia, harufu kutoitoa,
Kunuka kukapungua, vumbi ukishakuwa,
Watu kuvumilia, japo asili wajua,
Kila anayetumiwa, kwa hiari yake mwenyewe,
Moto anauchochea
Hawezi kusamehewa
Nadra ataombewa
Hata na anayemtumia
Jehanamu huingia!

Haramu ilokuwa, halali haitokuwa,
Na wanaonunuliwa, watakiwa kujijua,
Si kwa yangu manufaa, ila moto kukimbia,
Kila anayetumiwa, kwa hiari yake mwenyewe,
Moto anauchochea
Hawezi kusamehewa
Nadra ataombewa
Hata na anayemtumia
Jehanamu huingia!

Roho wanapokutoa, haya utajionea,
Ziraili hukujia, usoni ana ghasia,
Ulikuwa ni udhia, naye anakuchukia,
Kila anayetumiwa, kwa hiari yake mwenyewe,
Moto anauchochea
Hawezi kusamehewa
Nadra ataombewa
Hata na anayemtumia
Jehanamu huingia!

Kuumbwa akujutia, ewe mwanaizaya,
Mwingine angezaliwa, watu angeliwafaa,
Busati umetumiwa, viatu kuvifutia?
Kila anayetumiwa, kwa hiari yake mwenyewe,
Moto anauchochea
Hawezi kusamehewa
Nadra ataombewa
Hata na anayemtumia
Jehanamu huingia!

Kila anayetumiwa, kwa hiari yake mwenyewe,
Moto anauchochea
Hawezi kusamehewa
Nadra ataombewa
Hata na anayemtumia
Jehanamu huingia!

Kwa hasira hukutoa, hiyo roho yako mbaya,
Na hata ukijutia, motoni unaingia,
Naye huchekelea, sawasawa imekua,
Kila anayetumiwa, kwa hiari yake mwenyewe,
Moto anauchochea
Hawezi kusamehewa
Nadra ataombewa
Hata na anayemtumia
Jehanamu huingia!

Hili sijashabikia, wanangu ninawambia,
Mwataklwa kujikomboa, muache kuwa malaya,
Itawaghasi dunia, na akhera kuumia,
Kila anayetumiwa, kwa hiari yake mwenyewe,
Moto anauchochea
Hawezi kusamehewa
Nadra ataombewa
Hata na anayemtumia
Jehanamu huingia!

Usia nimeshatoa, babu sasa nimekua,
Vipofu wasiokua, haya watajionea,
Na viziwi watapewa, ishara wakalijua,
Kila anayetumiwa, kwa hiari yake mwenyewe,
Moto anauchochea
Hawezi kusamehewa
Nadra ataombewa
Hata na anayemtumia
Jehanamu huingia!

No comments: