Monday, March 26, 2012

Mashahidi mashairi

Mashahidi ushairi, Yarabi ndiyo dhamiri,
Inshallah kujiri, kwa yako hiyo kadiri,
Sitaki umashuhuri, nataka yako akheri,
Mashahidi mashairi, kwa vizazi vya akheri!

Mengine ninaghairi, ila yako wewe kheri,
Ni hadhari, ni khabiri, siwezi fanya jeuri,
Ni mchache wa kiburi, wala sina ujibari,
Mashahidi mashairi, kwa vizazi vya akheri!

Ushahidi nahadhiri, kwa yako kubwa fahari,
Yajaze yangu kwa heri, kaumu itasawari,
Ni elimu naabiri, kufata yako amrii,
Mashahidi mashairi, kwa vizazi vya akheri!

Hakuna ninalokariri, bila ya kwako Barrii,
Ni mtumwa sighairi, kazi yako idhihiri,
Nisiwe nami kuffari, kwangu uovu ujiri,
Mashahidi mashairi, kwa vizazi vya akheri!

Naishika bilauri, kunywa ni yako hiari,
Ya watu nisihasiri, na taifa taksiri,
Ila kama yako siri, waiondosha ghururi,
Mashahidi mashairi, kwa vizazi vya akheri!

Sina siri ni dhahiri, za wazi zangu habari,
Ninamuomba Ghaffuri, mengine yasije jiri,
Anayabuni mushawari, mazuri na yenye kheri,
Mashahidi mashairi, kwa vizazi vya akheri!

No comments: