HATA wakiwa wabaya, ndio juu walokuwa,
Ya kwao huyaamua, maovu na yakufaa,
Na kote huyasikia, ila wasipochagua:
Wakubwa wakiwa juu, ndio wanaosikika:
Kwetu hapa Afrika,
Mtunzi ana siku yake,
Nayo Mzungu amsome,
Kama sio kaburini!
Hunukuu na kutwaa, vya watu kuvitumia,
Na utu wakauvua, heshima kutoitoa,
Wakafanya wayajua, na ndio wayazindua,
Wakubwa wakiwa juu, ndio waonekanao:
Kwetu hapa Afrika,
Mtunzi ana siku yake,
Nayo Mzungu amsome,
Kama sio kaburini!
Mtunzi hatolilia, wala kuyapigania,
Kipaji alichojaliwa, wote huwagawia,
Hana wa kumbagua, wote kwake abiria:
Wakubwa wakiwa juu, ndio waonekanao:
Kwetu hapa Afrika,
Mtunzi ana siku yake,
Nayo Mzungu amsome,
Kama sio kaburini!
Ushetani wazidia, vya watu kuvitumia,
Na asante kutotoa, wala shukrani kutia,
Na Mola aangalia, ajua pakujalipia:
Wakubwa wakiwa juu, ndio waonekanao:
Kwetu hapa Afrika,
Mtunzi ana siku yake,
Nayo Mzungu amsome,
Kama sio kaburini!
Vyombo huviparamia, vya kwao visivyokuwa,
Miliki wakachukua, hata na mapato pia,
Na wanaoajiriwa, kazi yao kusifia:
Wakubwa wakiwa juu, ndio waonekanao:
Kwetu hapa Afrika,
Mtunzi ana siku yake,
Nayo Mzungu amsome,
Kama sio kaburini!
Bora wanaochangia, hutwangwa na kufukiwa,
Ni nafaka watumia, na pumba kuziachia,
Na leo kisichong'aa, kioo hakitakuwa,
Wakubwa wakiwa juu, ndio wanaosikika:
Kwetu hapa Afrika,
Mtunzi ana siku yake,
Nayo Mzungu amsome,
Kama sio kaburini!
Utumbo watautoa, kazi njema itakuwa,
Pasiwe na la kufaa, ila kashfa na waa,
Ila wanaotumiwa, rangi watazidishia:
Wakubwa wakiwa juu, ndio waonekanao:
Kwetu hapa Afrika,
Mtunzi ana siku yake,
Nayo Mzungu amsome,
Kama sio kaburini!
Uongo hutanzuliwa, kama ukweli ikawa,
Na wengine kuzomewa, ndio uongo wazua,
Na haya wasivyokuwa, hawajali umbuliwa:
Wakubwa wakiwa juu, ndio wanaosikika:
Kwetu hapa Afrika,
Mtunzi ana siku yake,
Nayo Mzungu amsome,
Kama sio kaburini!
Kona watazitumia, gia wakashikilia,
Wawe waliopotea, ni kweli waliotoa,
Nao wakatamaniwa, wakweli wameshakuwa:
Wakubwa wakiwa juu, ndio waonekanao:
Kwetu hapa Afrika,
Mtunzi ana siku yake,
Nayo Mzungu amsome,
Kama sio kaburini!
Hukaa kufikiria, ya ulua na murua,
Watu akawapatia, wajifunze na kujua,
Ila huwa ni unaa, watu kujitiatia,
Wakubwa wakiwa juu, ndio waonekanao:
Kwetu hapa Afrika,
Mtunzi ana siku yake,
Nayo Mzungu amsome,
Kama sio kaburini!
Ial huwa ni unaa, watu kujitiatia,
Wajifanye waelewa, na maana waijua,
Ila kwao ni ruia, haichelewi potea,
Wakubwa wakiwa juu, ndio waonekanao:
Kwetu hapa Afrika,
Mtunzi ana siku yake,
Nayo Mzungu amsome,
Kama sio kaburini!
Wakati utafikia, kizazi kikazaliwa,
Na kikija kufukua, hekima huichimbu,
Na busara wakatwaa, na nchi wakaiumua,
Wakubwa wakiwa juu, ndio waonekanao:
Kwetu hapa Afrika,
Mtunzi ana siku yake,
Nayo Mzungu amsome,
Kama sio kaburini!
Ila hawajayajua, ghaibu yaliyokuwa,
Kitabu chazidi jaa, uovu ulozagaa,
Na siku ikfikia, hukumu wataipewa:
Wakubwa wakiwa juu, ndio wanaosikika:
Kwetu hapa Afrika,
Mtunzi ana siku yake,
Nayo Mzungu amsome,
Kama sio kaburini!
Mtunzi akifichua, kwao ni mbaya huwa,
Watamshindilia, na kisha kumkandia,
Na watu wasiojua, wasijue ya kujua:
Wakubwa wakiwa juu, ndio waonekanao:
Kwetu hapa Afrika,
Mtunzi ana siku yake,
Nayo Mzungu amsome,
Kama sio kaburini!
Machi 01, 2012
Dar es Salaam. Tanzania.
Thursday, March 1, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment