Sunday, March 11, 2012

Sultani twawataka?

Sultani nashangaa, wanarudi Tanzania,
Mlango wanapitia,wa nyuma ulokuwa,
Baba fukara akiwa, cheo tena hutopewa,
Ufalme Tanzania, na uchifu twakataa?

Mkubwa asipokuwa, mzazi wa kukuzaa,
Cheo tena hutopewa, hupewa wanayemjua,
Sultani huzaliwa, na sio kuchaguliwa,
Ufalme Tanzania, na uchifu twakataa?

Chama kimedhamiria, wa kwao kuwachagua,
Baba wanaowajua, viongozi walokuwa,
Nje anayetokea, hawezi kukubaliwa,
Ufalme Tanzania, na uchifu twakataa?

Fedha asiyejaliwa, hawezi kuhurumiwa,
Fakiri kwao udhia, ushindi huukataa,
Mwenye nacho atapewa, asonacho hatofaa,
Ufalme Tanzania, na uchifu twakataa?

Na wanaowashangilia, chao waliochukua,
Mkoano hukataliwa, mtupu uliokuwa,
Nayo ni historia, yatokea Tanzania,
Ufalme Tanzania, na uchifu twakataa?

Nayo ni historia, yatokea Tanzania,
Ubepari kuingia, wajamaa walokuwa,
Na vyeo kupigania, kuzidi kujilimbikia,
Ufalme Tanzania, na uchifu twakataa?

Ujamaa umezaa, ubepari wenye doa,
Uliojaa ubaya, aidha na roho mbaya,
Hakuna kuhurumiwa, wakubwa wapate jaa,
Ufalme Tanzania, na uchifu twakataa?

Visiwa vinazaliwa, kwa mali vilivyojaa,
Katikati vimekaa, walo ndani maridhia,
Watu wa kuchaguliwa, kama si kuteuliwa,
Ufalme Tanzania, na uchifu twakataa?

Haya nawahadithia, ila mnayaelewa,
Hampati fikiria, kipimo mkachukua,
Uamuzi kuutoa, nchi utakaoifaa,
Ufalme Tanzania, na uchifu twakataa?

Tajiri nawaambia, hawezi kuangalia,
Masikini walokuwa, kwenye shida kuwatoa,
Yake huyaangalia, na zaidi kuongezewa,
Ufalme Tanzania, na uchifu twakataa?

Na chama kinachojaa, matajiri walokuwa,
Mwisho kitajaishia, katika kununuliwa,
Watu vyeo wakapewa, kwa bei watakayotoa,
Ufalme Tanzania, na uchifu twakataa?

Machi 11, 2012
Dar es Salaam. Tanzania.

No comments: