Sunday, March 11, 2012

Haramu hukumbatia

VIUMBE waliolaniwa, huachi kuwatambua,
Haramu hukimbilia, halali wakaikimbia,
Mazuri huyachukia, mabaya kufurahia,
Haramu hukumbatia, halali wakakimbia!

Muumini ninalia, ukweli huu kujua,
Khalifa twaangamia, kazi tunaichezea,
Tumeacha angalia, nyumba twaziporomoa,
Haramu hukumbatia, halali wakakimbia!

Ya kafiri na nasara, sasa yetu yamekuwa,
Kisha twashangilia, hata wao kuzidia,
Mja ninateketea, moto ninavyouhofia?
Haramu hukumbatia, halali wakakimbia!

Yetu tunayaachia, maovu twakumbatia,
Na wakali tunakua, kila tukikumbushiwa,
Maimamu wahofia, sadaka hamtatoa?
Haramu hukumbatia, halali wakakimbia!

Wengine wanababia, ya watu wasiojua,
Dini yao wachukia, hawataki isikia,
Eti ni uharamia, yaichukia dunia?
Haramu hukumbatia, halali wakakimbia!

Majina wayakataa, ya dini waliyopewa,
Ya kafiri wachukua, ili wapte sifiwa,
Na kisha wakadhaniwa, manasara wamekuwa,
Haramu hukumbatia, halali wakakimbia!

Kamba tuaniachia, wazazi na wana pia,
Kiingereza twakijua, Kiarabu twafulia,
Chema kilichochaguliwa, eti sie twakikataa?
Haramu hukumbatia, halali wakakimbia!

Nani atapigania, dini ya Murtaalia,
Juu akainyanyua, na beramu kupepea,
Vijana msipokuwa, kwayo mliozaliwa ?
Haramu hukumbatia, halali wakakimbia!

Wakati umewadia, kusimama kidedea,
Dini yetu kujivunia, kial tunapotembea,
Na ushindi kutimia, tuliokwishaahidiwa,
Haramu hukumbatia, halali wakakimbia!

Yote haya ayajua, Kadari alishatoa,
Mola anazingatia, vingine haitakuwa,
Na wanaozainiwa, hao kweli wapotea,
Haramu hukumbatia, halali wakakimbia!

No comments: