Monday, March 26, 2012

Feri imeshatushinda

Uongo utatuua, ukweli tuambiane,
Ya feri tunayoona, lipi mwataka mjuwe?
Twatakiana mabaya, wala hakuna kingine,
Feri imeshatushinda, uranium tutaiweza?

Mamluki mlokuwa, ni lazima tuwabane,
Taifa bado kukua, tusifanyane wajane,
Kubaleghe twatakiwa, ndio vichwa viumane,
Feri imeshatushinda, uranium tutaiweza?

Wengi tumeshawajua, maneno yenu manene,
Tena sana mwaongea, mkishakosa matone,
Rahisi kwenu kuua, kwa kuzitafuta 'mane',
Feri imeshatushinda, uranium tutaiweza?

Shahidi najichagua, na vizazi niungane,
Hadhari kukusudia, hadharani niinene,
Mhanga ninajitoa, watoto wasiuane,
Feri imeshatushinda, uranium tutaiweza?

Ikifaa kungojea, hata ikiwa karne,
Lipi lichimbwalo latufaa, hebu kwa wazi mnene,
Kumi mwaisifiwa, hakika nyie senene,
Feri imeshatushinda, uranium tutaiweza?

Trilioni zatakiwa, kwa ubia tuungane,
Na kama wajitetea, kwa hizo zao mashine,
Waziwazi nawambia, twendeni kwa wengine,
Feri imeshatushinda, uranium tutaiweza?

Wachina ninawajua, inafaa tuungane,
Mzungu ni haramia, vinginevyo tusimuone,
Anajifanya kujua, kumbe anatupa mavune,
Feri imeshatushinda, uranium tutaiweza?

Majuha waloobakia, nao hawa waungane,
Nchi zao zinaliwa, wao chao wakivune,
Uchungu hawakujaliwa, wataka wao wanone,
Feri imeshatushinda, uranium tutaiweza?

Feri wangeliijua, haya ni budi waone,
Haramu mwazungumzia, kubwa kama hii niione,
Najua haitakuwa, upele wenu mkune,
Feri imeshatushinda, uranium tutaiweza?

No comments: