Saturday, March 10, 2012

Watu wa maneno mengi

Katika dunia hii, maneno sasa maudhi,
Watu wameyakinai, kusikiza hawawezi,
Watu wataka kurai, uongo hawana ngozi,
Watu wa maneno mengi, ila vitendo ni ZIRO!

Hawateti buibui, lakini wafanya kazi,
Utando haustahi, ni mauti kwao nzi,
Na riziki si nishai, huifaidi wakazi,
Watu wa maneno mengi, ila vitendo ni ZIRO!

Ni miaka ya hajui, elimu haimalizi,
Ya kujifanya mjui, kwa kuiba ya watunzi,
Zama zao makidai, japo wafunga kitanzi,
Watu wa maneno mengi, ila vitendo ni ZIRO!

Ni miaka ya usui, haiba isiyo enzi,
Wanaodhani uhai, ni ngomayao maswezi,
Wazipigao nao, japo hali hawawezi,
Watu wa maneno mengi, ila vitendo ni ZIRO!

Si zama za makarai, kwa watu kitu hufunzi,
Watu wataka kusihi, maoni na utandawazi,
Ukiwa utandawizi, watafanya fumanizi,
Watu wa maneno mengi, ila vitendo ni ZIRO!

Adimu mchaichai, twanya visivyo azizi,
Hulka inachodai, kisichopo hakiwezi,
Litabaki kama fui, lisilo nalo mjenzi,
Watu wa maneno mengi, ila vitendo ni ZIRO!

Ndoo maji haijai, chini hakuna ulinzi,
Asiyesamehe mwui, hambariki mwenyenzi,
Na yake huwa jinai, Jaji asiwe mjuzi,
Watu wa maneno mengi, ila vitendo ni ZIRO!

Maisha ni maslahi, na wala si maongezi,
Hili asiyestahi, hana ya watu mapenzi,
Hujuza ni msanii, hawezi weka makazi,
Watu wa maneno mengi, ila vitendo ni ZIRO!

Maneno ni ulaghai, vinginevyo ni ushuzi,
Kama kitu hayafai, wala yako huongezi,
Ni bora kuyakinai, ujali yako makazi,
Watu wa maneno mengi, ila vitendo ni ZIRO!

Mkazi hategemei, cha nje apate makuzi,
Chake atakisabahi, na hatofanya ajizi,
Ina hadhi njia hii, mengine yote ushenzi,
Watu wa maneno mengi, ila vitendo ni ZIRO!

No comments: