Monday, March 26, 2012

Hutowahadaa wote

Uongo waliozoea, wataka jirahisishia,
Vyombo kwa kuvitumia, wadhani watafanikiwa,
Gizani tungelikuwa, hili ningelihofia,
Sikuzote, pande zote, watu wote ni vigumu:
Wote kuwadanganya!

Simu sasa zaoangea, ukweli utaujua,
Kwa masafa huchanua, vijijini kuingia,
Wazee wanayajua, hata na watoto pia,
Sikuzote, pande zote, watu wote ni vigumu:
Wote kuwadanganya!

Picha zinasimulia, kwingine yanayotokea,
Senegal nilijua, kifaransa kuwaambia,
Babu wakamchezea, na wakamtosa pia,
Sikuzote, pande zote, watu wote ni vigumu:
Wote kuwadanganya!

Mnachokipuuzia, ndicho kitawaumbua,
Akili zimechanua, Tanzania ni maua,
Vijana rangi wazua, kwa fani na tasnia,
Sikuzote, pande zote, watu wote ni vigumu:
Wote kuwadanganya!

Nyota wanachipukia, kuuliza wanaojua,
Uongo kuuukataa, na wakubwa kutumiwa,
Kwao demokrasia, azizi imeshakua,
Sikuzote, pande zote, watu wote ni vigumu:
Wote kuwadanganya!

Vizee vilivyokuwa, ndivyo mmeachiwa,
Njaa inavovisumbua, na fani wasiozijua,
Kama walivyolemaa, ndivyo mtavyolemaa,
Sikuzote, pande zote, watu wote ni vigumu:
Wote kuwadanganya!

Mhando mmemwachia, dungayembe mwachukua,
Mtavuna msiyojua, na chenfga kuambulia,
Sana nawasikitikia, njia mnavyopotea,
Sikuzote, pande zote, watu wote ni vigumu:
Wote kuwadanganya!

No comments: