Monday, March 26, 2012

Mazishi si kampeni

HAPA kwangu kupitia, Kisasi utamjua,
Jina kati yake mia, Qudusi aliyopewa,
Kila ukizingatia, maana yamechukua,
Mazishi si kampeni, Kisasi muogopeni!

Maqilla pia kapewa, srarehe azijua,
Si utani nakwambia, na wala sintakutania,
Na yeye ananijua, napenda kumlilia,
Mazishi si kampeni, Kisasi muogopeni!

Ajua namhofia, hasira akiingia,
Ila akifurahia, nataka mkaribia,
Nani wa kumchezea, kama baba alokuwa?
Mazishi si kampeni, Kisasi muogopeni!

Lakini si kwa udhia, kwa usafi kutokuwa,
Na mahala patakiwa, mwenyewe unapokuwa,
Mchezo kwangu ni dua,kila siku huitoa,
Mazishi si kampeni, Kisasi muogopeni!

Wapo wanaotania, hadhira ilipokuwa,
Laiti wangelijua, kisasi watafanyiwa,
Wenyewe wangekimbia, stara kuigombea,
Mazishi si kampeni, Kisasi muogopeni!

Siasa wanaotia, pale isipotakiwa,
Kama simu kutumia, masjidi ukiingia,
wanatembea na kaa, moto linaloungua,
Mazishi si kampeni, Kisasi muogopeni!

Riha yakataliwa, kwangu sintokarirbia,
Dhaifu nimeshakua, nani wa kuniangalia,
Hadi nitaporejea, kwa Mola wangu Jalia,
Mazishi si kampeni, Kisasi muogopeni!

No comments: