NDIVYO mlivyoamua, nami nawahudumia,
Kipendacho twaambiwa, nyama mbichi hutumia,
Na mie nimeridhia, wenyewe ninawaachia,
Mwataka nazi si tui, hali wali haifai?
Kaida naikubalia, ubishi sintoingia,
Wajua wanaojua, ya watu hawatasikia,
Mustakabali huwa, na sio uliokuwa,
Mwataka nazi si tui, hali wali haifai?
Ila ninavyoijua, desturi haijawa,
Tui ndilo hutumiwa, wali kujaupikia,
Nazi inapotakiwa, wenyewe wanayajua,
Mwataka nazi si tui, hali wali haifai?
Pengine yai likawa, mganga keshawaambia,
Maajabu hutokea, siwezi kuwabishia,
Macho ninaangalia, ibra zikitokea,
Mwataka nazi si tui, hali wali haifai?
Siwezi kuyakataa, wengine wamejaliwa,
Huruka wasio mbawa, hadi juu wakapaa,
Huzama wasioogelea, hadi chini kutembea,
Mwataka nazi si tui, hali wali haifai?
Haya nayazingatia, na watu kuwaachia,
Pembeni ninapokaa, si kama nasinzia,
Kila linalotokea, siachi kuangalia,
Mwataka nazi si tui, hali wali haifai?
Kuna zinazochimbiwa, kisha zikafukuliwa,
Kazi yake wanajua, wanapoyaagizia,
Kutabana humegua, kama sio kuugua,
Mwataka nazi si tui, hali wali haifai?
Uchovu nausikia, mengi sintowaambia,
Nawacha kufikiria,ajabu iliyokuwa,
Na wanaonielewa, wasisite kunambia,
Mwataka nazi si tui, hali wali haifai?
Sunday, March 4, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment