Tuesday, March 6, 2012

Kuna pweza Tanzania

Kuna pweza Tanzania, sikuhizi katokea,
Utabiri autoa, kwa yatakayotokea,
Hupenda kutangazia, watu wengi kusikia:
Kuna pweza Tanzania, mengi anatabiria:
Na mengi yasisimua!



Pweza mbali kaanzia, utabiri kuutoa,
Asema itatokea, mwongo mkweli akawa,
Kisha wasiojaliwa, matajiri wakuwa:
Kuna pweza Tanzania, mengi anatabiria:
Na mengi yasisimua!

Pweza anaendelea, utabiri kuutoa,
Mwizi ataheshimiwa, na mwema kuumbuliwa,
Haki itanunuliwa, hata raia kuua:
Kuna pweza Tanzania, mengi anatabiria:
Na mengi yasisimua!

Ardhi itahodhiwa, na wazawa wasokua,
Kila kitu kuchukua, ruksa wataipewa,
Hakuna cha kubakia, ila deni na balaa:
Kuna pweza Tanzania, mengi anatabiria:
Na mengi yasisimua!

Walinzi jambazi kuwa, laweza likatokea,
Askari kwogopewa, raia wakakimbia,
Mumiani walokuwa, malaika kudhaniwa:
Kuna pweza Tanzania, mengi anatabiria:
Na mengi yasisimua!

Watazuka wenye njaa, viongozi Tanzania,
Jethwa tukamshangaa, uchu asivyojaliwa,
Hata mfu kutumia, na mifupa kusagiwa:
Kuna pweza Tanzania, mengi anatabiria:
Na mengi yasisimua!

Wenye elimu kuvia, hilo linateegmewa,
Ubingwa ukapweleya, hata kudharauliwa,
Wasiojua wakawa, wataalamu waaminiwa:
Kuna pweza Tanzania, mengi anatabiria:
Na mengi yasisimua!

Mwana hatoajiriwa, wa masikini akiwa,
Na vyeo wakajapewa, wakubwa waliozaa,
Na uchumi wakapewa, fukara watumwa wakawa:
Kuna pweza Tanzania, mengi anatabiria:
Na mengi yasisimua!

Usultani warejea, katika kofia mpya,
Milki kutawaliwa, na wanaoteuliwa,
Fukara wakaachiwa, mapori yaliyovia:
Kuna pweza Tanzania, mengi anatabiria:
Na mengi yasisimua!

Maji yatatukimbia, milimani kurejea,
Na mvua kuanzia, chini zisikotokea,
Na ardhi kuungua, bila sababu kujua:
Kuna pweza Tanzania, mengi anatabiria:
Na mengi yasisimua!

Utu utalaaaniwa, na uungwana kuvia,
Kelele watasikia, ishirini kwa masaa,
Hospitali zikawa, madisko na mabaa:
Kuna pweza Tanzania, mengi anatabiria:
Na mengi yasisimua!

Umeme utalemaa, na kiguru kuja kuwa,
Ukashindwa kutembea, kwenye yetu mitaa,
Ikawa kubwa ngekewa, kwa vibaka walojaa:
Kuna pweza Tanzania, mengi anatabiria:
Na mengi yasisimua!

Hasira zitasambaa, hadi anga kufikia,
Na jua likajikwaa, na chini kuja kutua,
Wengine wakawa mkaa, kama si jivu kubakia:
Kuna pweza Tanzania, mengi anatabiria:
Na mengi yasisimua!

Mikoa itatumbuliwa, pasiwe cha kubakia,
Na juzi waliohamia, makazi yao yakawa,
Nao waliozaliwa, haraka kuondolewa:
Kuna pweza Tanzania, mengi anatabiria:
Na mengi yasisimua!

Udini utajifua, na wafu kuwafufua,
Mizuka ikatokea, katika yetu mitaa,
Rwanda kuihadithia, wakati inaendelea:
Kuna pweza Tanzania, mengi anatabiria:
Na mengi yasisimua!

Watoto watasambaa, katika hii dunia,
Nyumbani kutorejea, ila kwa kuamriwa,
Uraia kukataa, na mwengine kuchukua:
Kuna pweza Tanzania, mengi anatabiria:
Na mengi yasisimua!

No comments: