Biashara kitu chema, nchi ikishadidia,
Mazingira kuwa memea, kuingiza na kutoa,
Na katika takrima, mengine ikayalea:
Pato si tu biashara, bali na huduma pia,
Na kuzalisha tambua, kila kitu kuanzia,
Nchi inayozubaa
Kipato hakitakuwa
Na uchumi kwendelea!
Biashara kuchanua, usafiri watakiwa,
Ndege zinazochukua, mizigo kuzipania,
Iwe si tu abiria, hapo hapo kuishia:
Pato si tu biashara, bali na huduma pia,
Na kuzalisha tambua, kila kitu kuanzia,
Nchi inayozubaa
Kipato hakitakuwa
Na uchumi kwendelea!
Biashara kutanua, hadi mipakani kuwa,
Msumbiji na Zambia, Burundi na Rwanda pia,
Na Kongo kuivamia, Tip Tip kurejea:
Pato si tu biashara, bali na huduma pia,
Na kuzalisha tambua, kila kitu kuanzia,
Nchi inayozubaa
Kipato hakitakuwa
Na uchumi kwendelea!
Uganda kuangazia, Sudani tukaingia,
Na Kenya kuipatia, makwapani kuitia,
Hapo kweli tutakuwa, vidume vinavyojua:
Pato si tu biashara, bali na huduma pia,
Na kuzalisha tambua, kila kitu kuanzia,
Nchi inayozubaa
Kipato hakitakuwa
Na uchumi kwendelea!
Usafi tukiazimia, ni uwekezaji pia,
Meremeta nakwambia, watu watakuzengea,
Sio uchafu kujaa, jiji likawa kinyaa:
Pato si tu biashara, bali na huduma pia,
Na kuzalisha tambua, kila kitu kuanzia,
Nchi inayozubaa
Kipato hakitakuwa
Na uchumi kwendelea!
Huduma hazitokuwa, wachafu tukishakuwa,
Hunuka na kukataliwa, hata na wasozaliwa,
Bahati twaichezea, uongozi kulegea:
Pato si tu biashara, bali na huduma pia,
Na kuzalisha tambua, kila kitu kuanzia,
Nchi inayozubaa
Kipato hakitakuwa
Na uchumi kwendelea!
Sunday, March 4, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment