Thursday, March 8, 2012

Ukishindwa hauwezi

UNAPOWEZESHWA weza, ukishindwa hauwezi,
Watakiwa kutengeza, mambo ukayamaizi,
Ukajua kuyatunza, na yawe hayakukwazi,

Unatakiwa kutunza, ikawa haujikwazi,
Mambo ukayachunguza, yasiwe ni jinamizi,
Ukawa waendeleza, usilale usingizi,
Ukishindwa hauwezi, ukishawezeshwa weza!

Kama usipoyaweza, sio ya kwako saizi,
Hayo yatakuburuza, ikawa kwako ajizi,
Bure yakakuchakaza, usiwe unabarizi,
Ukishindwa hauwezi, ukishawezeshwa weza!

Mbegu hujapandikiza, yatakiwa maandalizi,
Na ukishapandikiza, wapaswa kuwa mtunzi,
Kitu kukiendeleza, kinahitaji malezi,
Ukishindwa hauwezi, ukishawezeshwa weza!

Pasiwe cha kubakiza, katika yake makuzi,
Kila unachokianza, kinahitaji darizi,
Na juu ukakikuza, lazima kupanda ngazi,
Ukishindwa hauwezi, ukishawezeshwa weza!

Akili ukichokoza, utakuwa ni mjenzi,
Lakini zikipooza, kitu haupandikizi,
Utabakia kucheza, na kupoteza kizazi,
Ukishindwa hauwezi, ukishawezeshwa weza!

Uwezo kweli kuweza, vinginevyo ni ajizi,
Mtaji wataka funzwa, ili uote mizizi,
Makubwa wanaofanza, lazima kuwa watenzi,
Ukishindwa hauwezi, ukishawezeshwa weza!

Siwezi kuendeleza, hili la sasa zoezi,
Mengine natetngeneza, ninaomba kunradhi,
Pengine nikijiweza, kesho nimalize kazi,
Ukishindwa hauwezi, ukishawezeshwa weza!

No comments: