Saturday, March 3, 2012

Wajinga wakiamka

Wajinga wakiamka, ukweli wakaujua,
Werevu hutatizika, wakaanza kufulia,
Mapigo yatawafika, wasiweze kuzuiya,

Wajinga wakiamka, werevu wako shakani!



Wajinga waking'amua, kulogwa hawakufanziwa,
Ila akili watwaa, ujinga wakawatia,
Nazo zimeisharejea, yabaki kuzitumia,
Wajinga wakiamka, werevu wako shakani!

Akili watatumia, dhulum kuiondoa,
Hujua walizaliwa, na akili zilojaa,
Ila zimeshindiliwa, zikaacha kuwafaa,
Wajinga wakiamka, werevu wako shakani!

Sasa wakizifumua, huru zipate kuwa,
Kila kitu watajua, na kuona yao njia,
Mjanja atakimbia, kubaya kuelekea,
Wajinga wakiamka, werevu wako shakani!

Umoja wakitambua, ndio waliochezea,
Macho wakishafungua, ukweli wakaujua,
Watazidisha umoya, hadi nyumbani ukawa,
Wajinga wakiamka, werevu wako shakani!

Dhifa wataziamua, maskani kufikia,
Makundi yatakatulia, na yao kuongelea,
Na mipango kuamua, ya mema yanayotakiwa,
Wajinga wakiamka, werevu wako shakani!

Huunda wakafanzia, vyombo vilivyotimia,
Kila kitu kupangia, na mikakati kutia,
Na siku ikitimia, huwa yasiyofikiriwa,
Wajinga wakiamka, werevu wako shakani!

Asubuhi kufikia, kila mtu hushangaa,
Hawa ndio walozubaa, mfukoni tukawatia,
Vipi wamejichomoa, sasa wanatuangazia?
Wajinga wakiamka, werevu wako shakani!

Hunyanyua vilivyokuwa, chini vimeshaingia,
Na juu wakajengea, juu zaidi wakawa,
Na miradi ikatua, waumini kujifaa,
Wajinga wakiamka, werevu wako shakani!

Tajiri hunyanyua, fukara wliokuwa,
Kamba wakashikilia, wote juu wakapaa,
Mola huwazawadiwa, mazuri yaliyokuwa,
Wajinga wakiamka, werevu wako shakani!

Dua akazipokea, na zaidi kuwafaa,
Na kila wanapokaa, pamoja nao hukaa,
Yakafana yalokuwa, zamani yamefubaa.
Wajinga wakiamka, werevu wako shakani!

Mazuri huzaliwa, kwa wema yakalelewa,
Dini wakaitambua, na nafasi kuiridhia,
Mmoja inayojua, Muumba aliyekuwa,
Wajinga wakiamka, werevu wako shakani!

Nafasi walioachiwa, huja ikawapotea,
Mbali wakajabakia, inda zikawazidia,
Na Falaki kutojua, mizengwe huwaumbua,
Wajinga wakiamka, werevu wako shakani!

Siku ikishatimia, ukweli tutaujua,
Wengi wanaowaabudia, wasije kitu kufaa,
Mikononi kuishiwa, liwezalo wasaidia,
Wajinga wakiamka, werevu wako shakani!

No comments: