Saturday, March 31, 2012

Chemchemi ikikauka

Mnagombea kitu gani, kisima hakina maji,
Nikifanya tathmini, hakuna mnachohitaji,
Na ujio siuoni, ila kuhama kijiji,
Chemchemi bila maji, mnagombea kitu gani ?

Nawaona Kisauni, bado mwatafuta m aji,
Walio kaskazini, sasa wawapeni uji,
Kiu hakiuamini, bado chalilia maji,
Chemchemi bila maji, mnagombea kitu gani ?

Na nyie Mchikichini, yako wapi mahitaji,
Mnauchoma ubani, wageuka kuwa mboji,
Bado yako ughaibuni, kwenu yasita hayaji,
Chemchemi bila maji, mnagombea kitu gani ?

Nimeuliza yamini, kama kuna ufujaji,
Yakawa bila thamani, tokea kwenye thaluji,
Wanasema yumkini, kwa hili si wasomaji,
Chemchemi bila maji, mnagombea kitu gani ?

Chemchemi bila maji, mnagombea kitu gani ?

Nimefika na Uzini, nilipotoka Kimbiji,
Utafiti kubaini, kisa chake ukosaji,
Na majibu si yakini, ila kuna uhitaji,
Chemchemi bila maji, mnagombea kitu gani ?

Nauliza Mkoani, na Chake kwenye mji,
Wao wayaficha ndani, mvua wakitaraji,
Watakuwamo shakani, ikiwa nayo haiji,
Chemchemi bila maji, mnagombea kitu gani ?

Malindi nikasaini, na Lamu nimewahoji,
Nauliza kuna nini, maji yakwama Buruji,
Au wapuuza dini, kakasirika wao Jaji?
Chemchemi bila maji, mnagombea kitu gani ?

Wanateta hadharani, bandari wanaitaraji,
Kama si leo mwakani, na nasara waundaji,
Kisiwa kiko shakani, Maajid kumsujudi,
Chemchemi bila maji, mnagombea kitu gani ?

No comments: