Saturday, March 24, 2012

Hivi unaweza kula

Kujivunga si tabia, jembe siiti vingine,
Na mja ni mazoea, yalivyo mambo ninene,
Hujua ukinijua, ni mimi sio mwingine,
Chakula, mavi pembeni, hivi unaweza kula!

Yakera yenye udhia, kwa nguchu nayo matone,
Hasa wawili mkiwa, kwenye raha na mavune,
Halafu mmoja akawa, mwenziwe asimkune,
Chakula, mavi pembeni, hivi unaweza kula!

Huja ikavia ndoa, kwa kila jambo ugune,
Imani ikapotea, mioyo itimuane,
Ikaingia balaa, daima msipatane,
Chakula, mavi pembeni, hivi unaweza kula!

Kila unachoamua, kikafanyika vingine,
Nawe ukiangalia, muamana usione,
Ukawa unajutia, heri ya kuwa mjane,
Chakula, mavi pembeni, hivi unaweza kula!

Kamba ukaiachia, ndipo ndoto ziachane,
Chakula ukitengewa, ni kinyesi ukione,
Matapishi kuachia, sakafu isuguane,
Chakula, mavi pembeni, hivi unaweza kula!

Au vingine ikawa, kwa uchafu kifanane,
Na nzi kuwagundua, usiku waonekane,
Hali bado wasinzia, wanga msielewane,
Chakula, mavi pembeni, hivi unaweza kula!

No comments: