Monday, March 26, 2012

Kushangaa si vibaya

Binadamu yake hulka, mapya kuyashangaa,
Likisha kufahamika, kawaida linakuwa,
Kisha hudharaulika, likaacha kujaliwa,
Kushangaa si vibaya, ubaya kuyaharibu!

Ubaya wenye hakika, kupuuza yalokuwa,
Yakaacha kujengeka, uzee yakaingia,
Yawe yasahaulka, na kaburi kuchimbiwa,
Kushangaa si vibaya, ubaya kuyaharibu!

Reli zilishajengeka, wakati tunashangaa,
Uhuru tukaushika, wa bendera kupepea,
Na leo zinameguka, uzee zimeshaingia,
Kushangaa si vibaya, ubaya kuyaharibu!

Vipi zilisahaulika, kosa letu kushangaa,
Hazikukarabatika, ovyo tukaziachia,
Na sasa twashtukia, zapaswa kujengwa upya,
Kushangaa si vibaya, ubaya kuyaharibu!

Barabara zajengeka, nadra kuangalia,
Akili zimeteguka, hatujui fatilia,
Kila kitu chafanyika, kama vile hai chawa,
Kushangaa si vibaya, ubaya kuyaharibu!

Nani wa kuangalia, waziri hajamjua,
Kama ameshamjua, hajui fuatilia,
Mikenge tunaingia, nchi yazidi lemaa,
Kushangaa si vibaya, ubaya kuyaharibu!

Visima vinachimbika, hakuna kuangalia,
Hadi vaja kubomoka, hakuna anayejua,
Na shule zinajengeka, udhaifu ziliizojaa,
Kushangaa si vibaya, ubaya kuyaharibu!

Na shule zinajengeka, udhaifu ziliizojaa,
Wajenzi wanaumbuka, mabomu zikizinduliwa,
Wenyewe wastahika, na wakubwa wahamiwa,
Kushangaa si vibaya, ubaya kuyaharibu!

No comments: