Sunday, March 11, 2012

Wazee wakiridhika

NCHI ya kubarikiwa, wazee huangalia,
Wala haitawatumia, kwa zaini na sanaa,
Ila lazima ikiwa, nalo hilo walijua,
Wazee wakiridhika, nchi huneemeka!

Nchi hii yaumia, wazee kutojaliwa,
Ni wana wanaachiwa, fukara kuangalia,
Watoto wasipokuwa, maisha kizaazaa,
Wazee wakiridhika, nchi huneemeka!

Radhi inatukimbia, nafsi kutupalia,
Ya kwetu kuangalia, ya kwao yawe yaviaa,
Utu umetupotea, roho mabya zimekuwa,
Wazee wakiridhika, nchi huneemeka!

Mateso yawaumbua, na dhiki zilivyojaa,
Kula kwao kubabia, na afya yao hatia,
Nani wa kuwaangalia, nchi ikishakataa?
Wazee wakiridhika, nchi huneemeka!

Na aibu tusokuwa, twenda kuwakimbilia,
Ya kwetu kuwaambia, na yasiyowasaidia,
Mimi hili nashangaa, tena ninalikataa,
Wazee wakiridhika, nchi huneemeka!

Uzee tungetambua, ndoo mizizi huanzia,
Imara wasipokuwa, nchi yote huungua,
Na kinachobakia, majivu tu yatakuwa,
Wazee wakiridhika, nchi huneemeka!

Hili ninaling'amua, siachi wanyenyekea,
Masikini walokuwa, kila wanaponijia,
Kidogo nikakitoa, kwa hali kuwajulia,
Wazee wakiridhika, nchi huneemeka!

Nchi ingelitambua, hazina iliyokuwa,
Vyema ikiwatumia, mbali twaweza fikia,
Kadri kuinyanyua, nchi yetu Tanzania,
Wazee wakiridhika, nchi huneemeka!

Bashiri twamlilia, wazee kusaidia,
Nafuu kwao ikawa, huko tunakoendea,
Na nchi ikajaliwa, mamboye kutengenea
Wazee wakiridhika, nchi huneemeka!

No comments: