Monday, March 26, 2012

Mwangoja limiwa shamba?

Vibaya mmelelewa, sikuzote kufanyiwa,
Wengi mmeshalemaa, ya kwenu yadidimia,
Kisa eti mwangojea, mtu kuja wafanzia,
Mwangoja limiwa shamba, mavuno yawe ya nani?

Mithali naitumia, shamba kama tungekuwa,
Tungoje kuja limiwa, na mbegu tukagawiwa,
Ni ajabu ingekuwa, njaa kutokujatuua,
Mwangoja limiwa shamba, mavuno yawe ya nani?

Serikali haijawa, hivyo mnavyoidhania,
Tajiri ingelikuwa, kodi isingechukua,
Kwani ingejitegenea, na tena kutusaidia,
Mwangoja limiwa shamba, mavuno yawe ya nani?

Serikali yetu njaa, tulimacho yategemea,
Na kodi inazopewa, na viwanda vilokuwa,
Bishara nazo pia, kwa kodi huzichangia,
Mwangoja limiwa shamba, mavuno yawe ya nani?

Na migodi yatakiwa, kuacha zao sanaa,
Si tu kodi kutoa, bali mapato kugawa,
Ni yetu Watanzania, vingine watuibia,
Mwangoja limiwa shamba, mavuno yawe ya nani?

Huu mtaji ukiwa, zana tukazinunua,
Shambani tukiingia, vitu tutajifanyia,
Miaka haitazubaa, nchi bora itakuwa,
Mwangoja limiwa shamba, mavuno yawe ya nani?

Kila mtu atakiwa, akili kuzitumia,
Kitu ukafikiria, maishani kukufaa,
Sahau ninakwambia, kuja tena ajiriwa,
Mwangoja limiwa shamba, mavuno yawe ya nani?

Kihamba ukishapewa, kulima unatakiwa,
Ardhi jana ilikuwa, leo akili twapewa,
Ubongo kuutumia, maisha yakachanua,
Mwangoja limiwa shamba, mavuno yawe ya nani?

Usingoje kulimiwa, wala kuja hudumiwa,
Anza kuchachamaa, masomoni unapokuwa,
Fikra kuziangua, kwa mayai ya kufaa,
Mwangoja limiwa shamba, mavuno yawe ya nani?

Moja moja kuchagua, huku chuo waingia,
Hadi ukimalizia, ajira umeshafyatua,
Muajiri utakuwa, na wala sio mwajiriwa,
Mwangoja limiwa shamba, mavuno yawe ya nani?

No comments: