Monday, March 26, 2012

Kinyesi njiani.....

UTUSANI natumia, tena kwa kukusudia,
Vipofu waliokuwa, pengine watajizomea,
Uvivu wakiachia, matatizo wakajua,
Chakula, pembeni mavi, hivi utaweza kula ?

Kipato mwakusudia, kua au kupungua?
Wasafi msipokuwa, ndoto yenu itakuwa,
Maneno mwajivunia, vitendo vimepotea?
Chakula, pembeni mavi, hivi utaweza kula ?

Hoteli zanyanyuliwa, ni uyoga zimekua,
Pembeni ukisogea, kinyesi kinaelea,
Mzungu katumbukia, na laana kaitoa,
Chakula, pembeni mavi, hivi utaweza kula ?

Hamkioni kinyaa, wakubwa mlokuwa,
Ulaya mnaingia, ya kwao mwajionea,
Hivi ndivyo inavyokua, au mmepungukiwa?
Chakula, pembeni mavi, hivi utaweza kula ?

Njia kunao udhia, nao pia wa kinyaa,
Huwezi ijua njia, kila pembe yatumiwa,
Pikipiki zashtua, hujui zinakotokea,
Chakula, pembeni mavi, hivi utaweza kula ?

Kama kinyesi balaa, na bajaji nazo pia,
Popote hujipitia, hata za miguu njia,
Hatuioni sheria, mitaa yetu nazaa,
Chakula, pembeni mavi, hivi utaweza kula ?

Madiwani watumbua, enzi wameshaipewa,
Kazi yao kupokea na si haki kutoa,
Wepesi wa kuchukua, sio wa kuangalia,
Chakula, pembeni mavi, hivi utaweza kula ?

Ukubwa ukililia,jua ni kutumikia,
Wakubwa walokuwa, wataka kutumikia,
Sultani wamekua, chini hawatatembea,
Chakula, pembeni mavi, hivi utaweza kula ?

Ya kwao si ya raia, wanao wa kutumiwa,
Watu wa kuagiziwa, utumwa walojitia,
Hawajengi, wabomoa, sasa tunajionea,
Chakula, pembeni mavi, hivi utaweza kula ?

No comments: