Tuesday, March 27, 2012

Uongozi kudhibiti

Uongozi kizingiti, ndani unajifukia,
Hahujui wakati, wala yanayotokea,
Husiikiliza pointi, ovyo zilizonukuliwa,
Uongozi kudhibiti, na sio kudhibitiwa!

Hupewa kisicho nati, na kisha kikaachia,
Haufanywi utafiti, kwenye giza hubakia,
Na kusaoma magazeti, ni wavivu walokuwa,
Uongozi kudhibiti, na sio kudhibitiwa!

Tivii nazo wavuti, husakura kwa kinyaa,
Wataka kitu smati, ndani kipate tulia,
Hakuna tena wakati, ya zamani kurudia,
Uongozi kudhibiti, na sio kudhibitiwa!

Redio hawazifati, wajinga huwaachia,
Huwasoma Muqsiti, akayafanza sawia,
Baina kati kwa kati, huja wakatumbukia,
Uongozi kudhibiti, na sio kudhibitiwa!

Huwajaza Muqliti, hekima watarajiwa,
Na siku yao umati, juu huja wanyanyua,
Tena bila masharti, mtu aliyeyatoa,
Uongozi kudhibiti, na sio kudhibitiwa!

Nchi yatakiwa chati, na miundo kutumia,
Ikawa jambo hukuti, mtu lisilopangiwa,
Kila kitu kwa wakati, kikawa chahudumiwa,
Uongozi kudhibiti, na sio kudhibitiwa!

Taifa lataka dhati, kila kitu kufuatia,
IKawa hakuna kiti,kisichokupekuliwa,
Na zikatoka ripoti, yafaa au kutofaa,
Uongozi kudhibiti, na sio kudhibitiwa!

Nchi haifurukuti, bila ya kusimamiwa,
wako watu kama nati, lazima kufunguliwa,
Kisha kubanwa kwa kati, hapo hapo kutulia,
Uongozi kudhibiti, na sio kudhibitiwa!

Wapo wasio nishati, vigumu kwenda sogea,
Wataka pigwa mabuti, watoke walipokaa,
Na wengine kama sleti, kazi ni kuandikiwa,
Uongozi kudhibiti, na sio kudhibitiwa!

Upo wa gari na wa jeti, mnapaswa kuchagua,
Upo ujuzi na cheti, na vyote haviwi sawa,
Na uhai na mauti, mwaweza hayo chagua,
Uongozi kudhibiti, na sio kudhibitiwa!

No comments: