Monday, March 26, 2012

Samaki waanza kuoza, pakachani wabakia?

Kwa mamia wanaoza, samaki kwenye pakacha,
Uoza wafululiza, kama vile wapikicha,
Juu utajitokeza, asubuhi kumekucha,
Kwenye pakacha samaki, nusuye wameshaoza:
Wewe umejituliza,
Hivi utaacha kuoza?

Samaki nawauliza, mbona bado mwajificha ?
Mngemuomba muweza, mngeacha Ualinacha,
Wenyewe kujigeuza, kabla hamjachacha,
Kwenye pakacha samaki, nusuye wameshaoza:
Wewe umejituliza,
Hivi utaacha kuoza?

Mazoea yawakwaza, kuchoropoka mwakacha,
Wenyewe mwajimaliza, pakacha msipoacha,
Maana budi kuoza, hili hatwezi waficha,
Kwenye pakacha samaki, nusuye wameshaoza:
Wewe umejituliza,
Hivi utaacha kuoza?

Hunuka wanaooza, tena huwezi kuficha,
Thamani mtajikwaza, uoga kuwachekecha,
Hadhi mkailemaza, mkabakia machicha,
Kwenye pakacha samaki, nusuye wameshaoza:
Wewe umejituliza,
Hivi utaacha kuoza?

Watu watawapuuza, toka mguu hadi kichwa,
Wengine kuwaeleza, mmeshakuwa ndondocha,
Au sokoni mwauza, kama vile ni mchicha,
Kwenye pakacha samaki, nusuye wameshaoza:
Wewe umejituliza,
Hivi utaacha kuoza?

Mwanunuliwa ni viza, mayai kwenda pikicha,
Kutupa kwenye jeneza, ndani mlilolificha,
Na shaibu na ajuza, msukule kuwaficha,
Kwenye pakacha samaki, nusuye wameshaoza:
Wewe umejituliza,
Hivi utaacha kuoza?

Sina nililobakiza, na samaki sio pacha,
Ila nimewajuliza, wacheze lao chakacha,
Au wasipoliweza, basi iwe hiyo chachacha,
Kwenye pakacha samaki, nusuye wameshaoza:
Wewe umejituliza,
Hivi utaacha kuoza?

No comments: