Wednesday, March 21, 2012

Tabaka la watawala

Kubali usikubali, hii sasa yetu hali,
Sura tumeibadili, twajali wana na wali,
Twazipuuza akili, tunatumia miili,
Tabaka la watawala, wengine watawaliwa!

Hii ni ardhilhali, kwayo nchi yake hali,
Nautoa ufadhili, niseme yalo kamili,
Ukweli yangu asili, uongo kwangu aghali,
Tabaka la watawala, wengine watawaliwa!

Ni sukari na pilipili, maisha yetu wawili,
Wapo walio na hali, na wasiokuwa hali,
Mapambano kukabili, kila mtu bilkuli,
Tabaka la watawala, wengine watawaliwa!

Ni nchi ya madalali, wenye kiu na njaakali,
Kujihami bilkuli, au hugeuzwa mali,
Ardhi ikawa chali, ukaikosa halali,
Tabaka la watawala, wengine watawaliwa!

Ni nchi ya wadahili, kwa hesabu nazo mali,
Wakosa bei anzali, wajanja wakihimili,
Hugeuzwa baradhuli, uongo zao kauli,
Tabaka la watawala, wengine watawaliwa!

Kuna wana wa halali, na wasio wa halali,
Usultani wajali, si uzazi ila mali,
Na wetu mustakabali, kitanzi tabaka mbili,
Tabaka la watawala, wengine watawaliwa!

Ni kama pacha wawili, tofauti kwazo hali,
Na mmoja ni bahili, ala peke yake mali,
Na mwenzie hastahili, aidha hatohimili,
Tabaka la watawala, wengine watawaliwa!

Ninanena kulhali, hili budi kubadili,
Na tusipolibadili, Tsumani haiko mbali,
Mtaikumbuka kauli, wimbi tukishakabili,
Tabaka la watawala, wengine watawaliwa!

No comments: