Wednesday, March 21, 2012

Mwana kuwa kama mwana

Si waja wa kujasana, viumbe wanapishana,
Na huu wetu ubwana, tabia zafarakana,
Hakubali muungwana, hulka kutopishana,
Mwana kuwa kama baba, hili muhali naona!

Mbona twalemaa sana, na fikra zagandana,
Nani atakwa utwana, na wengine wawe mabwana,
Hili kwangu gumu sana, kumeza nina hiana,
Mwana kuwa kama baba, hili muhali naona!

Mbeleko hatukuchana, tunazidi kubebana,
Wengine wageni wana, ya mji wataungana?
Kuoa ni kufaana, na sio kufungamana!
Mwana kuwa kama baba, hili muhali naona!

Nywele mjenzi kitana, na wembe huongozana,
Na kazi sio kujuana, ila kuafikizana,
Mambo yataka kufana, na sio kuteuana,
Mwana kuwa kama baba, hili muhali naona!

Nchi yataka pishana, sio kusukumizana,
Watu usawa wanena, dawa si kupuuzana,
Milango kufungiana, mwisho mtaburuzana,
Mwana kuwa kama baba, hili muhali naona!

Watu wataka amana, na kisha kuwezeshana,
Kijiti kupokezana, ni riadha kubanana,
Hili angalizo sana, hawajlisoma mabwana,
Mwana kuwa kama baba, hili muhali naona!

Mambo ni kuchambuana, na sio kuchaguana,
Na raundi haiwi kona, haziwezi kufanana,
Na maji sura hayana, na nuru yatafanana,
Mwana kuwa kama baba, hili muhali naona!

Hesabu si kutoana, ipo kujumlishana,
Na sana mkizidishana, mwisho kuna kugawana,
Hasimu hutafutana, hawana la kujengana,
Mwana kuwa kama baba, hili muhali naona!

No comments: