Saturday, March 31, 2012

Ukililia kiatu

KIATU ukililia, unapaswa kutambua,
Wapo waliozaliwa, miguu hawakupewa,
Hapungukiwi Jalia, ila hilo karidhia,
Ukililia kiatu, mwenzio miguu hana!

Mzazi hupungukiwa, unapaswa kulijua,
Ndiye anayezitoa, pindi anapojaliwa,
Kama asipogaiwa, ni kipi atakigawa?
Ukililia kiatu, mwenzio miguu hana!

Siwezi kujisifia, riziki ninaigawa,
Yapo juu alokuwa, nami ninamgonjea,
Hushukuru nikipewa, na kukosa naridhia,
Ukililia kiatu, mwenzio miguu hana!

Maisha yana hatua, kupata na kupotea,
Kama somo ukijua, sahihi na kukosea,
Na mengine majaliwa, hauwezi kuyajua,
Ukililia kiatu, mwenzio miguu hana!

Yako wewe angalia, na tosheka ukijua,
Wako juu watakuwa, nawe kati kubakia,
Na chini wakafatia, kama wewe wasojaliwa,
Ukililia kiatu, mwenzio miguu hana!

Mwana ninakuusia, jenga kinaya na dunia,
Na hautopungukiwa, utatosheka radhia,
Yao ukaangalia, na yako ukatumia,
Ukililia kiatu, mwenzio miguu hana!

Tosheka nayo dunia, nayo itakuachia,
Nje wanaoangalia, na husuda kuwajaa,
Husumbuka na dunia, kufa bado wana njaa,
Ukililia kiatu, mwenzio miguu hana!

Huwa watu wa kulia, kucheka wakakohoa,
Maji hawawezi tia, kinywani wametulia,
Shinikizo huingia, mapema kuteketea,
Ukililia kiatu, mwenzio miguu hana!

Akili ukijaliwa, wapaswa kuzitumia,
Fakiri ukijijua, juu zitakunyanyua,
Na subira ukilea, inshallah utajaliwa,
Ukililia kiatu, mwenzio miguu hana!

No comments: