WABANTU ninawajua, kisichozaa udhia,
Hata wangelihamia, na kutulia Ulaya,
Kuzaa kwao ngekewa, asiyezaa huvia,
Lisofaa hamng'oi, mwang'oa chenye kufaa ?
Na vipi kisichozaa
Uchungu kuusikia
Na mbeleko kushonewa?
Nchi wanaoshikilia, ugumba wakishakua,
Uzazi kutoujua, yepi yao manufaa?
Ila ninashangaa, watu kuwavumilia,
Lisofaa hamng'oi, mwang'oa chenye kufaa ?
Na vipi kisichozaa
Uchungu kuusikia
Na mbeleko kushonewa?
Kupanda lisilofaa, mara ukishalijua,
Kung'oa hutochelewa, mara moja hili huwa,
Mbali ukaliambaa, lifaalo kulitwaa,
Lisofaa hamng'oi, mwang'oa chenye kufaa ?
Na vipi kisichozaa
Uchungu kuusikia
Na mbeleko kushonewa?
Siyo yakuchekelea, haya ya kusikitikia,
Na yanayowafikia, hujifanya wanajua,
Ila washinda kujua, hawajui kujijua,
Lisofaa hamng'oi, mwang'oa chenye kufaa ?
Na vipi kisichozaa
Uchungu kuusikia
Na mbeleko kushonewa?
Muda huwapotezea, hao waliowachagua,
Ugumba kuudhania, utakuja kupotea,
Miaka kuangukia, pasiwe la kutokea,
Lisofaa hamng'oi, mwang'oa chenye kufaa ?
Na vipi kisichozaa
Uchungu kuusikia
Na mbeleko kushonewa?
Kidogo kilichokuwa, nacho pia hupotea,
Ikatoweka ngekewa, nyumba mikosi kujaa,
Kila siku pakavia, na watu kupakimbia,
Lisofaa hamng'oi, mwang'oa chenye kufaa ?
Na vipi kisichozaa
Uchungu kuusikia
Na mbeleko kushonewa?
Ila waongo wakiwa, mwana watamnunua,
Na ksiha kusingizia, eti wamekwishajaliwa,
Uongo wakatarazia, watu kutokuujua,
Lisofaa hamng'oi, mwang'oa chenye kufaa ?
Na vipi kisichozaa
Uchungu kuusikia
Na mbeleko kushonewa?
Mwana hujaambiwa, kamlamba alomzaa,
Kila ukiangalia, sura hujaitambua,
Kila siku anakua, na ibra kazaliwa,
Lisofaa hamng'oi, mwang'oa chenye kufaa ?
Na vipi kisichozaa
Uchungu kuusikia
Na mbeleko kushonewa?
Hubaki kushangilia, nafusi wasiojua,
Maziko yawe kuzaa, mbwembwe pia na nazaa,
Malengo kutofikia, na lango kutofungua,
Lisofaa hamng'oi, mwang'oa chenye kufaa ?
Na vipi kisichozaa
Uchungu kuusikia
Na mbeleko kushonewa?
Sunday, March 4, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment