Sunday, March 11, 2012

Mwizi ni mwizi

WAPO waibao wazo, nao pia huwa wezi,
Huwa ni wao mchezo, ya wengine wachuuzi,
Akili ni hamnazo, wanangoja ya uwizi,
Hata mwizi wa mawazo, na yeye pia ni mwizi.

Hawakupewa uwezo, ya kwao yote ni wizi,
Hujifanya matangazo, na kazi hawaziwezi,
Hawakupata mafunzo, vipi wawe wajuuzi?
Hata mwizi wa mawazo, na yeye pia ni mwizi.

Huzuka kama igizo, sifa zao kudarizi,
Ikiwa wataka nguzo, ukafanza egemezi,
Wakishapata penyezo, yako yote huwa wazi,
Hata mwizi wa mawazo, na yeye pia ni mwizi.

Wataiba kwa vigezo, ubia mwaja maizi,
Hukufanza angalizo, toka hapo huwawezi,
Huchukua yote dezo, wakafanza uvamizi,
Hata mwizi wa mawazo, na yeye pia ni mwizi.

Tungo pia zako nyenzo, hadithi na simulizi,
Wakazitia kikwazo, kwa dhuluma na hirizi,
Ikawa huna sogezo, na kheri hauimaizi,
Hata mwizi wa mawazo, na yeye pia ni mwizi.

Sanaa zetu ni bezo, haziwazuii wezi,
Zote hazina katazo, wala sheria na hadhi,
Kila mwenye dundulizo, kuiba kwake si kazi,
Hata mwizi wa mawazo, na yeye pia ni mwizi.

Hili ni letu tatizo, chini tuliobarizi,
Na wasio na uwezo, kupambana nao wezi,
Walindwa na wenye uwezo, kamwe kitu hauwafanzi,
Hata mwizi wa mawazo, na yeye pia ni mwizi.

Nafupisha maelezo,nukta mmemaizi,
Naleta changu chetezo, ubani kuutaradhi,
Nimwombe mwenye uwezo, kuzilinda zangu kazi,
Hata mwizi wa mawazo, na yeye pia ni mwizi.

No comments: