Monday, March 26, 2012

Uhai mwahuzunika

VIUMBE wanafiki, hebu Mola angalia,
Kwenye msiba mikiki, wadhani wafurahia,
Walokuwa hawafiki, wa kwanza wanaingia,
Uhai mwahuzunika, kifo mwasherehekea ?

Uko hai hushikiki, wote wankukimbia,
Wala hauaminiki, nani atakuridhia,
Ya kwako hawahusiki, ya kwao hushikilia,
Uhai mwahuzunika, kifo mwasherehekea ?

Huwa haueleweki, hawaijui tabia,
Ikiwa mbali hufiki, njia waliochagua,
Husemwa hutabiriki, hasara waweza tia,
Uhai mwahuzunika, kifo mwasherehekea ?

La kwako halijengeki, zaidi hulibomoa,
Kiumbe hakimiliki, hadi awe na madoa,
Roho hazivumiliki, na si ruksa kutoa,
Uhai mwahuzunika, kifo mwasherehekea ?

Kila kitu si riziki, SMS hutumiwa,
Mdogo haneemeki, mkubwa akivimbiwa,
Na mnyonge hanyongeki, hubaki kama udhia,
Uhai mwahuzunika, kifo mwasherehekea ?

Wengi hawafurahiki, maisha kwao ruia,
Huota hayakamiliki, mengine huchimbuliwa,
Fakiri hatamaniki, kwa wakubwa ni kinyaa,
Uhai mwahuzunika, kifo mwasherehekea ?

Wala hana taharuki, utajiri alopewa,
Au kwa cheo kukua, kikubwa kashikilia,
Hajui asiyemjua, na ndugu hunyanyapaa,
Uhai mwahuzunika, kifo mwasherehekea ?

Adhimu siwashtaki, hayo yao majaliwa,
Moto haukamiliki, bila mkaa kupewa,
Na ahali na rafiki, wengine kuni wakawa,
Uhai mwahuzunika, kifo mwasherehekea ?

Kiumbe hakamiliki, hadi kujiondokea,
Maisha yake hakiki, utakuta ni tanzia,
Ila wasio na dhiki, wachache wachaguliwa,
Uhai mwahuzunika, kifo mwasherehekea ?

Maisha hayashikiki, kwa wengi waliokuwa,
Na wasio wamiliki, ndio wajiendeshea,
Kugawa haigawiki, hadi machweo ya jua,
Uhai mwahuzunika, kifo mwasherehekea ?

Najua sistahiki, haya kujawambia,
Sikujali tawfiki, ugomvi naununua,
Mseme sieleweki, hadi kizazi kipya,
Uhai mwahuzunika, kifo mwasherehekea ?

No comments: