Saturday, March 24, 2012

Katika imani zao

Dunia inakinzana, viumbe wengi fitina,
Imani tena hamna, watu wanaogopana,
Si mabwana si watwana, wote sasa wafanana,
Katika imani zao, wapo wana wenye mwana!

Na walio juu sana,wanazidi kwa laana,
Uonao wa maana, kumbe maana hawana,
Na sasa wajulikana, nchi hazina amana,
Katika imani zao, wapo wana wenye mwana!

Imani sasa kuvuna, na madhambi kufichana,
Mabaya wafanyiana, hata huwezi kunena,
Kisa sheria kununa, aloamru Rabana,
Katika imani zao, wapo wana wenye mwana!

Hakuna mjanja sana, kumzidi Maulana,
Haya alishayaona, na yeye kasemwa sana,
Hata kumzulia wana, viumbe wake wa jana,
Katika imani zao, wapo wana wenye mwana!

Ssasa wanaibishana, na dunia wanayaona,
Kazi sasa wakazana, waja wema kutopatana,
Wasingizia hiyana, hadi ndugu twauana,
Katika imani zao, wapo wana wenye mwana!

Laiti tungeshikana, mchawi ajulikana,
Sisi naye kuumana, cha kweli kujulikana,
Imani yetu amana, angetuenzi Rabana,
Katika imani zao, wapo wana wenye mwana!

Lakini waovyo sana, wenyewe tunauana,
Mchawi keshatutukana,ya ovyo twadhaniana,
Haya yanauma sana, tumuombe Rahmana,
Katika imani zao, wapo wana wenye mwana!

Kwanini twamalizana, na yetu yanafanana,
Ni nani mbora sana, mbona hatujaulizana,
Na alye juu sana, atatupa muamana?
Katika imani zao, wapo wana wenye mwana!

Hapa twaangamizana, na pepo hatutaiona,
Kisa ni wabaya sana, yetu hayana maana,
Yanamuudhi Rabana, huu sio uungwana,
Katika imani zao, wapo wana wenye mwana!

No comments: