Wednesday, March 21, 2012

Asili yangu kimya

Mkimya nimezaliwa, umbeya sikuzoea,
Siasa sikujaliwa, ubishi ninahofia,
Maneno nikitumia, mwenyewe ninaumia,
Asili yangu kimya, nikisema nakosea!

Wengi wanikazania, mdomo kuufungua,
Jambo sikufikiria, siwezi zungumzia,
Ni malezi nimepewa, vingine kwangu balaa,
Asili yangu kimya, nikisema nakosea!

Kwa watu nayasikia, mengi wakiyaongea,
Ila siwezi chukua, ushahidi siupewa,
Naona nasingizia, watu nisiowajua,
Asili yangu kimya, nikisema nakosea!

Wala hili sikunuia, lenyewe limetokea,
Bora pekee kukaa, umbeya nikakimbia,
Sioni kinachonifaa, ila dunia kinyaa,
Asili yangu kimya, nikisema nakosea!

Ya watu sitaki jua, sembuse kuyasikia,
Kiumbe namkataa, ila kwa njema ridhaa,
Ujumbe aliyepewa, nje ya hii dunia,
Asili yangu kimya, nikisema nakosea!

Kitabu najisomea, tulichokwishashushiwa,
Wengi tusiokijua, wala kukiangalia,
Maongezi huongea, moyo wangu ukatua,
Asili yangu kimya, nikisema nakosea!

Asubuhi hufungua, sura nikatembelea,
Na kila nikikinyanyua, kitu kipya hupewa,
Siri nyingi kimejaa, wachache wanaojua,
Asili yangu kimya, nikisema nakosea!

Redio ninazisikia, dini zikishangilia,
Mmoya aliyekuwa, wengi wanamsifia,
NI mwenye kutwangalia, viumbe tunamjua,
Asili yangu kimya, nikisema nakosea!

Daawa zinazitoa, zenye njema majaliwa,
Machozi yakanitoa, mja nilivyopotea,
Pungufu nilivyokuwa, na shukrani kunywea,
Asili yangu kimya, nikisema nakosea!

Na familia wanajua, njia wananiachia,
Na wengine watambua, wema uliochanua,
Nao pia wameshakua, wakimya kwa mazoea,
Asili yangu kimya, nikisema nakosea!

Kelele huzikataa, ila ninazoletewa,
Wanasiasa wakawa, nje wanabishania,
Na wauza kuvamia, wakizinadi bidhaa,
Asili yangu kimya, nikisema nakosea!

Nayaomba majaliwa, ukimya kwendelea,
Ni hidaya ilokuwa, tukufu kukadiriwa,
Nami naishikilia, kwa wivu usiosinyaa,
Asili yangu kimya, nikisema nakosea!

No comments: