Tuesday, March 27, 2012

Kiongozi bandia

Kiongozi wa sumaku, anaweza kutulia,
Huvutwa huku na huku, nani wa kumshikilia,
Huwa kama vile kuku, mtama anayemwagiwa,
Na kiongozi bandia, hujaliwa itihari ?

Husikiza mamluku, uongo akavamia,
Akaifanya shauku, isivyo akaamua,
Na akangalia huku, mkuku wakatokea,
Na kiongozi bandia, hujaliwa itihari ?

Huwa achezeshwa zuku, sindima wakachagua,
Huja nyuma zake siku, kila leo kuchelewa,
Hana analolishuku, kila kitu hufanziwa,
Na kiongozi bandia, hujaliwa itihari ?

Hawezi kutabaruku, diniye anaigwaya,
Watu humpiga chuku, adhani wamshangilia,
Ukija mtafaruku, mwenyewe huja bakia,
Na kiongozi bandia, hujaliwa itihari ?

Huwa mwingi wa shauku, na machache hutimia,
Ahadi zake ni buku, mfukoni ana mia,
Yanavyozidi masiku, utapeli uhofiwa,
Na kiongozi bandia, hujaliwa itihari ?

Haishi bila ruzuku, inayotoka kubaya,
Na barua za udaku, nyuma huwa zafatia,
Japo anakula kuku, tembele hufurahia,
Na kiongozi bandia, hujaliwa itihari ?

Na akiwa na kasuku. upuuzi ataongea,
Hata yalo marufuku, watu atawaachia,
Haya huja kumpiku, hatimaye huzidiwa,
Na kiongozi bandia, hujaliwa itihari ?

Maisha si sikukuu, ila kwa waliopagawa,
Yako kama yako huku, mkenge umashaingia,
Na kisha siku ya siku, hatia ni kutumiwa,
Na kiongozi bandia, hujaliwa itihari ?

No comments: