Saturday, March 10, 2012

Kusema si uongozi

Mdomo alojaliwa, kawaida kuongea,
Kubwabwaja si hatia, hata kwa wasiojua,
Wapo waliojaliwa, nao wasiojaliwa,
Kusema si uongozi, waweza sema ushuzi!

Uongozi kutanzua, kisichofaa kufaa,
Hii ni yetu hatua, bora ukapalilia,
Kuoza na kujifia, ni watu kuwachezea,
Kusema si uongozi, waweza sema ushuzi!

Uongozi kutatua, na sio kuugulia,
Kila anayelilia, uongozi anapwaya,
Na asiyejitambua, vya ndani nje huvaa,
Kusema si uongozi, waweza sema ushuzi!

Kilemba anayevua, akaivaa kofia,
Jua amepungukiwa, na kaongeza udhia,
Hakuna kinachokaa, kiachiwe kisichokaa,
Kusema si uongozi, waweza sema ushuzi!

Watu anayechukia, kwa sura nazo tabia,
Kiongozi haijawa, na wala haitokuwa,
Huyo fani kavamia, kisebengo huachia,
Kusema si uongozi, waweza sema ushuzi!

Fani yataka kujua, hakika wanaojua,
Wasojua kuwajua, uwape wanaojua,
Na yao ukasikia, na tena kuzingatia,
Kusema si uongozi, waweza sema ushuzi!

Ujinga unapovia, wahaka huinukia,
Haya usipozingatia, kinyume chake huzua,
Watu wakakushangaa, na imani kupungua,
Kusema si uongozi, waweza sema ushuzi!

Mzuri hawezi kuwa, kazungukwa na wabaya,
Na uoza haijawa, uzuri ukachipua,
Hata Mola huchukiya, malaika huwatoa,
Kusema si uongozi, waweza sema ushuzi!

Mazingira yakivia, hata ukubwa hunywea,
Hubakia kama bua, wa chini kukutania,
Shere wakakufanyia, udhani wakuabudia,
Kusema si uongozi, waweza sema ushuzi!

Wapo wanaonyamaa, kazi wanaoijua,
Ni watu huwatumia, watu wanaowatumia,
Mengi sana kuyajua, kabla hawajaamua,
Kusema si uongozi, waweza sema ushuzi!

Kumi ukijifanyia, wao mia huamua,
Ufanifu huzidia, na ufanisi kukua,
Na ajaye kusifiwa, huwa juu ulokuwa,
Kusema si uongozi, waweza sema ushuzi!

No comments: