Tuesday, March 27, 2012

Uzee hauwi dawa

Kama sio majaliwa, uzee hauwi dawa,
Kila unavyojongea, huzidi uoza kuwa,
Tabia ikawa mbaya, na kwa wengine kinaya,
Uzee hauwi dawa, ikesha tabia mbaya!

Huongezeka tamaa, dhambi ukanyemelea,
Dhuluma ukachagua, na vitoto kuvizia,
Mvi japo zakujaa, huna aibu wala haya,
Uzee hauwi dawa, tamaa kuja pungua?

Uongo utauzua, mkeo ukamwambia,
Na watoto kudoea, chumo likikulemea,
Ukweli huukimbia, motoni kukimbilia,
Uzee hauwi dawa, uongo kuukataa !

Dini wasioijua, mikongojo watumia,
Hushindwa kumrejea, Mola anayewangojea,
Wakawa wanakimbilia, bado ya kwenye dunia,
Uzee hauwi dawa, Rabana kumrejea !

Na wenye tabia mbaya, kama wameshalaaniwa,
Hulka huendelea, h ata uzee kwingia,
Huwezi kumuongoa, silo alilopangiwa,
Uzee hauwi dawa, ikesha tabia mbaya!

Wapo wanaojitia, ujana waendelea,
Mambo wakajifanyia, ya kuchukiza raia,
Nishai wakawatoa, na heshima kupungua,
Uzee hauwi dawa, tamaa kuja pungua?

Waliokuwa wambeya, humazah huchimbua,
Ukubwani kuugua, na hasa ugonjwa ukawa,
Kila wataloongea, si lingine ni umbeya,
Uzee hauwi dawa, umbeyakuukataa !

Watu wakubwa wakiwa, huangamia dunia,
Kama wale wa Ulaya, nako Amerika pia,
Vizazi vyaumbuliwa, kwa umbeya kuzagaa,
Uzee hauwi dawa, Rabana kumrejea !

No comments: