Saturday, March 10, 2012

Ufakiri twautaka

KARATA waitumia, ushindi kujipatia,
Masikini kubakia, rahisi kutawaliwa,
Mtawala hukataa, utajiri kujaliwa,
Ufakiri twautaka, ili kula misaada!

Ndiyo yanayotokea, katika hii dunia,
Ufukara umekuwa, mifugo kuangalia,
Wanasiasa wabwia, usije kutokomea,
Ufakiri twautaka, ili kula misaada!

Usije kutokomea, maana unawafaa,
Fakiri kwa yake njaa, kila kitu uhofia,
Na mema huyakimbia, jahanamu akijua,
Ufakiri twautaka, ili kula misaada!

Ufakiri maridhia, huruma unaonewa,
Na misaada hupewa, Marekani na Ulaya,
Wao trilioni kutwaa, wakati unasinzia,
Ufakiri twautaka, ili kula misaada!

Wajua hawa majuha, kupewa wamezoea,
Cha kwao kukifukua, wengine wanaachia,
Na makombo waridhia, kila wanapogawiwa,
Ufakiri twautaka, ili kula misaada!

Ufukara ni sanaa, wakubwa waitumia,
Kila wanapoingia, kwa mabwana tarajiwa,
Hujiuza kwa ubia, nalo wakafagilia,
Ufakiri twautaka, ili kula misaada!

Nidhamu huwaishia, ukadhani changudoa,
Haya kuyafurahia, ijapo waja umia,
Aghalabu hulemaa, tena kutokutembea,
Ufakiri twautaka, ili kula misaada!

Ninawasikitikia, kwa wanaojiumbua,
Busara zimepungua, rahisi wakimbilia,
Aghali iliyokuwa, kwa nchi nao raia,
Ufakiri twautaka, ili kula misaada!

Amebakia Jalia, kadiri kuiondoa,
Nuksi nazo balaa, zisijekututokea,
Tunaomba Inshallah, hilo nalo lipate kuwa,
Ufakiri twautaka, ili kula misaada!

No comments: